Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Tanga, ulioongozwa na Mwenyekiti wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Abdulrahman Shiloow, umepitisha Rasimu ya Sheria ndogo za Halmashauri ya Jiji la Tanga za mwaka 2024, baada ya kuzijadili na kutoa mapendekezo ya maboresho kwa rasimu hiyo, ambapo zitakapo kamilika, zitafuta sheria ndogo zinazotumika sasa za mwaka 2014 na 2019.
Akifungua mkutano huo, Mstahiki Shiloow amesema, rasimu hiyo ni nyongeza ya vitu vidogo vidogo vilivyoongezwa kwenye sheria zinazotumika sasa, ambapo maboresho hayo yamefanywa ili kuendana na wakati, kuwezesha Halmashauri kutimiza wajibu wake wa kuihudumia jamii.
Akiwasilisha rasimu hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Kaimu Mwanasheria wa Jiji la Tanga, Idrisa Mbondera amesema utungaji wa sheria ndogo hizo umefuata utaratibu wa kisheria kama ulivyoainishwa kwenye kifungu cha 90 cha Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura 288.