Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ)
kwa kushirikiana na Idara ya Michezo, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Taasisi ya Maendeleo ya Mashirikiano ya Ujerumani (GIZ) na Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD), wataadhimisha ya siku ya
kimataifa ya Mtoto wa Afrika Juni 29, 2024 kwa kuandaa mashindano ya riadha kwa wanafunzi wa skuli mbalimbali za Zanzibar.

Maadhimisho hayo yatawahusisha jumla ya washiriki 150 ambapo kati ya hao wakiwemo wanafunzi 75 kutoka katika skuli za Unguja, wakilenga kuhamasisha usawa wa kijinsia katika michezo na kuwaleta pamoja wadau kutoka taasisi za kiserikali na zisizokuwa za
kiserikali, ikiwemo wanafunzi kutoka skuli mbalimbali za Unguja, wanamichezo,
walimu wa michezo, na wadau wote wa masuala ya usawa wa kijinsia.

Maadhimisho hayo, poa yanatoa fursa kwa wasichana kuonesha vipaji vyao na uwezo wao wa kushiriki katika michezo mbalimbali, pamoja na kujadili changamoto na vikwazo vinavyowazuia kushiriki katika michezo na kuhimiza uanzishwaji wa madawati ya jinsia katika taasisi za michezo.

Mashindano ya riadha yataanza saa 12 na nusu asubuhi, yakianzia maeneo ya Forodhani na yataishia katika viwanja vya Mnazi Mmoja Zanzibar yakishirikisha wanafunzi wa jinsia zote kutoka skuli mbalimbali za Unguja.

Kaulimbiu ya wadau katika maadhimisho ya mwaka huu ni “Wakati ni sasa! Wekeza katika elimu na michezo kwa watoto wote”. Tukio hili
linatarajiwa kuleta mwamko na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwapa nafasi sawa watoto wote kushiriki katika michezo, bila kujali jinsia zao.

Aidha, mashindano hayo pia yanatarajia kutoa washindi watatu zaidi Wanawake na watatu
wanaume na kutambuliwa rasmi ikiaminika kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuleta usawa wa kijinsia na kuwawezesha watoto wa kike na wa kiume kujifunza stadi za maisha, kujenga ujasiri, na kushirikiana kwa amani na kuheshimiana.

Kupitia taarifa ya Idara ya Mawasiliano ya TAMWA ZNZ, Wanahabari, wazazi, walezi, na wananchi wote wamealikwa kujitokeza kwa
wingi kushuhudia na kuunga mkono tukio hili la kihistoria katika kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha watoto wote kufikia ndoto zao katika Nyanja mbalimbali bila vizuizi vyovyote.

Changamoto za Wawekezaji: Serikali kujadiliana na mabalozi - Makamba
Uboreshaji afya: USA kizazi hodari kuwafikia Watoto zaidi ya laki moja