Swaum Katambo – Katavi.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amewataka wananchi kutumia fursa ya uwepo wa ofisi za Bima kupata elimu ya masuala ya Bima pindi wanapopatwa na majanga.

Mrindoko ameyasema hayo mara baada ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa ofisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Ziwa Tanganyika itakayotoa huduma kwa mikoa mitatu ya Katavi, Rukwa na Kigoma.

“Wananchi Katavi tumieni vizuri fursa hii ya uwepo wa ofisi za Bima Kanda ya Tanganyika,ni fursa nzuri kuhakikisha kila mwananchi anajielimisha na kutumia huduma za Bima kwa sababu wote tunafahamu kuwa Bima ni kinga ya janga lolote ambalo linaweza kukukuta bila kutarajia,” amesema.

Naye Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware amesema uelewa mdogo wa wananchi kuhusu masuala ya Bima mkoani Katavi umepelekea Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kuanza utaratibu wa kujenga ofisi ya Kanda ya Ziwa Tanganyika mkoani humo.

“Katavi ni Mkoa wa kimkakati kuna bandari ya Karema hapa,na tumeona mwamko kwa watu wa Kanda ya Ziwa Tanganyika haukuwa mzuri ukilingamisha na mikoa mingine, ndio maana tumeona tuwepo hapa ili kuwashawishi na kuwatangazia kuhusu fursa hii” amesema.

Hata hivyo Dkt. Saqware amesema uwepo wa ofisi hiyo utasaidia wananchi kuondokana na changamoto ya kwenda kupata huduma katika Kanda ya Magharibi mkoani Tabora huku Meneja wa Bima Kanda ya ziwa Tanganyika Kurenje Mbura akisema mpango walionao ni kuanza kutoa elimu kwa wananchi kupitia majukwaa mbalimbali.

“Tumeshakutana na viongozi mbalimbali wa Mkoa ili kuhakikisha wao kwanza wanakuwa na uelewa wa Bima kabla ya kuanza kufikia wananchi kupitia majukwaa mbalimbali.., mfano hapa juzi kulitokea majanga ya mafuriko watu walipata hasara mbalimbali ila wangekuwa na Bima wangekuwa na uwezo wa kufidiwa” amesema Mbura

Baadhi ya wananchi mkoani Katavi wamesema hawana uelewa kuhusu masuala ya Bima hivyo wameomba elimu ya masuala ya Bima itolewe mtaani.

“Tunasikia sikia tuu kwenye vyombo vya habari na vipeperushi mambo ya Bima ila kiundani hatuyaelewi,tunaomba kupatiwa elimu zaidi kuhusu hizo bima na faida zake”,amesema Hassan Ramadhan Mkazi waMpanda

Hata hivyo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inatarajia kuanza ujenzi wa ofisi za Kanda ya Ziwa Tanganyika katika Mkoa wa Katavi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 huku kwa sasa ikiendelea na shughuli zake katika jengo la kukodi lililopo mjini Mpanda.

Uteuzi: Dkt. Jafo Waziri wa Viwanda na Biashara
Kibiti: Kamati za usimamizi wa maafa zapewa mafunzo