Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amemteuwa Dkt. Selemani Jafo kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka imeeleza kuwa Dkt. Jafo aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) anachukua nafasi ya Dkt. Ashatu Kijaji ambaye naye ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Kabla ya uteuzi huu, Dkt. Kijaji alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara ambapo pia Rais Samia pia amemteuwa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba kuwa Katibu Mkuu wa Wizara yaMadini.
Mhandisi Samamba anachukua nafasi ya Kheri Mahimbali ambaye atapangiwa kazi nyingine, huku Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Yusuph Mwenda akiteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais, Ofisi ya Rais, Ikulu.