Bodi ya Sukari nchini Tanzania imesema msimamo wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuwalinda wananchi, wakulima, wawekezaji na wadau wengine muhimu kwa kuhakikisha inafanya maboresho makubwa kwa maslahi ya Watanzanaia wote.

Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania Profesa Kenneth Bengesi, aliwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku chache baada ya kupitishwa sheria mpya ya sukari nchini.

“Tunaendeleza majadiliano na wadau ili kutatua changamoto zote sambamba na kuikuza sekta ya sukari kwa sababu ni jambo nyeti na muhimu, hivyo tunalichukulia hili kwa umakini,” alisema Profesa Bengesi.

Kwa siku za karibuni kumekuwa na mijadala kadhaa kutokana na siku chache zilizopita kugubikwa na uhaba wa sukari hali iliyoibua hofu kwa Watanzania wote.

WAKATI HUO HUO

Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Kenneth Bengesi, amesema kitendo cha kampuni za wazalishaji kutoagiza sukari nje ya nchi katika msimu wa 2022/2023, kulisababisha bei ya sukari kupanda na kuongeza hali mbaya ya upatikanaji wa sukari nchini.

“Kampuni nne zilipewa vibali lakini ni kampuni moja tu ya Kilombero kati ya nne iliingiza sukari tani 2,380 licha ya wazalishaji kupewa vibali vya kuagiza sukari kwa msimu huo. Kitendo cha wazalishaji kutoingiza kiasi chote cha sukari kilichoidhinishwa 2022/23 kilisababisha upungufu na kupanda bei hadi kufikia shilingi 4,000 kwa kilo moja mwezi Juni, 2023,” alisema Profesa Bengesi.

Profesa Bengesi alisema kitendo cha kushindwa kwa wazalishaji kuingiza sukari katika msimu wa 2022/2023 kuliwapotezea sifa ya kisheria ya kupewa vibali kwa msimu wa 2023/2024, lakini bado serikali iliendelea kuwapa vibali vya kuendelea na shughuli ya uingizaji wa sukari nchini Tanzania.

Dkt. Feleshi aipongeza OSHA usimamizi sheria mahala pa kazi
Haya hapa maagizo ya Rais Samia kwa Dkt. Jafo