Swaum Katambo – Katavi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amempongeza Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA ) Mussa Ibrahim Mbura pamoja na watendaji wake kwa usimamizi mzuri wa maboresho ya jengo jipya la abiria linalojengwa katika Kiwanja cha Ndege Mpanda kilichopo mkoani Katavi.
Pongezi hizo amezitoa mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiserikali ambapo mara baada ya kuwasili Kiwanja cha Ndege Mpanda amekagua maboresho ya jengo jipya la abiria linalojengwa katika kiwanja hicho ambacho kinakwenda kutatua kero ufinyu wa eneo la kusubiria abiria wanaposafiri.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA ) Mussa Ibrahim Mbura amesema mradi huo ulianza kutekelezwa mnamo mwezi machi 2023 na unatarajia kukamilika ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Aidha Mbura amesema gharama za mradi hui ni shilingi bil 1.4 na mpaka sasa umefikia asilimia 95.
“Jengo la awali lilikuwa na uwezo wa kuchukua abiria 48 kwa wakati mmoja, Kutokana na shughuli za kiuchumi na kiutalii kukua katika Mkoa wa Katavi tuliamua kuchukua maamuzi chini ya Serikali yako kujenga jengo jipya, hili jengo sasa litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 240 na hii ni kutokana na shughuli za kiutalii hasa kuongezeka katika Mkoa wa Katavi,” amesema Mbura.
Nao baadhi ya wananchi wamefurahishwa na ujio wa Rais Dkt Samia Suluh Hassan ambapo wamesema ni mara ya kwanza kuja mkoani Katavi toka aingie madarakani.
Rais Samia yupo mkoani Katavi kwa ziara ya siku nne ambayo imeanza leo Julai 12 na inatarajia kukamilika Julia 15 huku akiwa mkoani humo anatarajiwa kukutana na kuongea na wazee wa Mkoa wa Katavi,Kutembelea kituo cha kupozea umeme wa Gridi ya Taifa Mlele.
Aidha pia atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha siku ya wazazi kitaifa na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Mpanda.