Swaum Katambo, Mlele  – Katavi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa mradi wa Gridi ya Taifa unakamilika ifikapo septemba mwaka huu.

Ameyasema hayo alipotembelea na kituo cha kupokelea, kupoza na kusambaza umeme cha Inyonga mkoani Katavi akiwa katika viwanja vya Shule ya Msingi Inyonga iliyopo Halmashauri ya Mlele mara baada ya kukagua na kujionea maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.

Kutokana na Mkoa wa Katavi unategemea umeme unaozalishwa kwa mafuta na mashine za jenereta na kupelekea changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, Rais Samia amepongeza hatua iliyofikiwa ya mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2019 ambao hadi sasa umefikia asilimia 97 na kuwahakikishia wananchi kuwa ifikapo mwezi septemba Mkoa wa Katavi utatumia umeme wa Gridi ya Taifa na kuachana na umeme wa Jenereta.

“Mtaachana na majenereta ambayo yanatumia pesa nyingi sana kama zaidi ya bilioni mbili kila mwezi kwa kuendesha majenereta na kuwasha umeme ndani ya Mkoa wa Katavi, Sasa tunakwenda kuachana na hayo na sasa tutatumia gridi ya Taifa,” amesema

Aidha, Rais Samia amewataka wananchi mkoani humo kutumia umeme huo kwa kuzalisha shughuli za kiuchumi pamoja kukuza uwekezaji ndani ya Mkoa huo kutokana na uwepo wa umeme wa uhakika.

“Ndugu zangu wa Mlele na Katavi, umeme huu ni gharama, nimesema fedha hapa kuna bilioni 48 ujenzi wa kituo, lakini bilioni 116 kujenga njia za usambazaji na kupokea umeme kwa hiyo umeme huo utakaokuja kutumiwa ulipwe kama mtu anavyotumia, umeme si huduma ni biashara lazima tulipe umeme ili uendelee kuwaka.”

Hata hivyo, amewataka TANESCO mara baada ya mradi huo wa Gridi ya Taifa kukamilika, kujipanga vyema katika usambazaji na uunganishaji wa umeme kwenye taasisi na majumbani.

Kadhalika, amewahakikishia wananchi wote waliotoa maeneo kwa ajili ya kupitisha mradi wa Gridi ya Taifa kulipwa fidia zao zote huku akiwashukuru kwa moyo walio uonesha wa kuruhusu mradi kupita kabla ya fidia.

“Tumelipa fidia nusu, nimeambiwa kuna kama bilioni 4 zaidi zinatakiwa za kuja kumalizia fidia niwahakikishie fidia ile tunakuja kuilipa,” alisema.

Taswira ya Miundombinu pamoja na Kituo cha kupoza, kupokea na kusambaza umeme wa Gridi ya Taifa kilichopo Inyonga Mkoani Katavi.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga alisema kuwa kwa sasa Serikali inatumia zaidi ya shilingi bilioni 2.2 kwa mwezi kwa ajili ya mafuta ya Dizeli kuzalisha umeme mkoani humo kwa kutumia majenereta.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko alisema tayari umeme wa REA umefika katika vijiji vyote 172 vya Mkoa huo hivyo umeme wa Gridi ya Taifa utatatua kabisa tatizo la Umeme mkoani humo.

Kwa upande wao wananchi wa Mkoa wa Katavi wamefurahishwa na ahadi ya Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ya kufikiwa na umeme wa Gridi ya Taifa ifikapo mwezi septemba mwaka 2024.

Mradi huo umegharimu zaidi ya bilioni 164 ambazo ni gharama za ujenzi wa kituo pamoja na kujenga njia za usambazaji na kupokea umeme.

Rais Samia ahudhuria Kilele Wiki ya Wazazi Kitaifa
Rais Samia: Acheni kuvamia maeneo ya hifadhi