Rais wa Rwanda, Paul Kagame ameshinda muhula wa nne wa kuiongoza nchi hiyo kufuatia uchaguzi wa urais na bunge uliofanyika Julai 15, 2024.
Katikq uchaguzi huo, jumla ya Wapiga kura milioni tisa walishiriki ambapo jumla ya kura milioni saba zilizokuwa zimehesabiwa, Kagame alipata asilimia 99.15 ya kura zote.
Mgombea wa Chama cha Green Party of Rwanda (DGPR), Frank Habineza yeye amepata asilimia 0.53 ya kura huku mgombea binafsi Phillipe Mpayimana akipata asilimia 0.32 za kura zilizohesabiwa.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Rwanda, Oda Gasinzigwa amesema zoezi la kuhesabu kura linaendelea, na hii leo Jumanne julai 16 yatatangazwa matokeo ya muda ya uchaguzi wa bunge.
Wakati wa Kampeni, Kagame ambaye ni Mwanajeshi kitaaluma alisema mara kadhaa kwamba angeshinda uchaguzi huo kutokana na mchango wake katika maendeleo ya Rwanda.
Katiba ya Rwanda ilifanyiwa mabadiliko mwaka 2015, ili kumuongezea Kagame haki ya kugombea mihula mingine miwili ya miaka mitano na ni wazi sasa ataliongoza Taifa hilo hadi mwaka 2029.