Johansen Buberwa – Kagera.
Kamati ya Uwezeshaji Bishara Kitaifa, imefika Mkoani Kagera kwa lengo la kutembelea vituo vya forodha, ili kujionea hali ya shughuli za uwezeshaji pamoja na biashara na upitishaji wa mizigo katika vituo hivyo.
Akizungumza katika kikao maalumu cha makaribisho ya Kamati hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Dkt. John Simbachawene amesema lengo ni kuchochea ukuaji wa uchumi kati ya Tanzania na mataifa jirani kupitia biashara.
Amesema, “Kamati yetu ya kitaifa ya uwezeshaji imefika mkoani Kagera kufuatilia takwa la mkataba wa uwezeshaji wa biashara ulisainiwa Januari 30 mwaka 2020 ambao unazungumzia umuhimu wa mataifa kuweka mazingira wezishi ya ufanyaji wa bishara ili kupunguza muda wa ufanyaji wa biashara baina ya mataifa yanayopakana na umuhimu wa taasisi za mipikani kushirikiana na mataifa katika ufanyaji wa biashara.”
Awali, akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajath Fatma Mwassa alisema Mkoa huo una vituo vya forodha rasmi sita, ambavyo kwa kiasi kikubwa vinachangia ukusanyaji wa mapato kutokana na bishara kutoka Tanzania kufikia zaidi watu milioni 300, kwa nchi za Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya, Sudan Kusini na DRC.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa chemba ya Wafanyabishara Kilimo na wenye Viwanda – TCCIA Mkoa wa Kagera, Rwechungura Mali alisema miongoni mwa changamoto zinazowakumba Wafanyabishara wa Mkoa huo ni tozo ndogo ndogo ambazo si halali zikiwemo za ushuru wa mazao wa soko kwenye mipaka.
Ziara ya kamati ya uwezeshaji Biashara kitaifa mkoani mkoani Kagera inatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku tatu katika vituo vya pamoja vya forodha, pamoja na Bandari ya Bukoba kuanzia Julai 16 hadi 19, 2024.