Meneja wa Shirika la Umeme Nchini, TANESCO Mkoa wa Pwani Eng. Cosmas Mkaka amekemea baadhi ya Wananchi wa Mkoa wa Pwani wanaojihusisha na vitendo vya wizi wa miundombinu ya umeme mkoani humo ambavyo husababisha kukatika kwa umeme na  hasara kwa Serikali.

Cosmas ametoa wito huo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake mjini Kibaha kuhusu changamoto ya wizi wa miundombinu ya umeme na kusema wizi huo husababisha shirika kuingia gharama ya kurekebisha miundombinu hiyo.

Amesema, “najua tumeshaongea viongozi wa serikali za mitaa vijiji na madiwani lakini niombe na Wananchi wengine wote ukiona Kuna dalili zozote zinazoweza kuharibu miundombinu wasisite kuwasiliana na uongozi wa Kijiji husika, vituo vya polisi au hata kutupigia simu tuweze kuokoa Mali ambayo ingeweza kuibiwa au kuharibiwa na tukapata hasara kubwa.”

Aidha Eng Mkaka ameshukuru Wananchi walioonyesha ushirikiano kwa kutoa taarifa mbalimbali za usalama wa miundombinu ya shirika hilo, huku akitoa wito kwa jamii pale itakapoona dalili zisizo njema kutoa taarifa, ili kusaidia kuokoa miundombinu.

“Tukiwajibika kulinda miundombinu yetu ambayo ni Mali yetu sote itatusaidia sisi sote kuwa na maendeleo katika mkoa wetu wa Pwani hivyo tusaidiane kwani inavyoharibiwa inaharibu Kodi za Wananchi, Mali ya umma,” alisema Eng. Mkaka.

Kalambo: Rais Samia azindua Jengo la Utawala la Halmashauri
Biashara Vituo vya Forodha: Kamati yawasili Kagera