Heldina Mwingira.

Kundi kubwa la Wanawake wanaoshiriki au kujishughulisha na mambo ya siasa hapa Nchini, mara nyingi hukabiliwa na ukatili mtandaoni.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Women at Web kwa kushirikiana na TAMWA, umebaini kuwa, asilimia 79 ya Wanawake Wanasiasa na Wanaharakati wa kisiasa, walifanyiwa ukatili wa kijinsia kwa njia ya mtandao, wakati wa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Tukiwa tunaelekea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, ni wazi kuwa kutaibuka vitendo vya ukatili wa mtandaoni unaolenga kuharibiana kisiasa.

Hata hivyo ikumbukwe kuwa mara nyingi ukatili wa mtandaoni huleta matokeo mabaya kwa mtu mmoja mmoja au jamii kwa ujumla na kupelekea athari kwa jamii, familia au Taasisi.

Kutokana na utafiti uliofanywa na Watetezi wa haki za Wanawake (WHRDs), unasema aina za athari zinazopatikana ni unyogovu, wasiwasi, wasiwasi kushiriki katika jamii anayoishi, na kujisikia huzuni.

Pia utafiti huo unaonesha kuwa, Wanawake wengi walipata ugonjwa wa mfadhaiko baada ya kiwewe (PTSD), kutokana na ukatili uliofanywa dhidi yao kupitia mitandao.

Katika kuangazia athari za ukatili dhidi Wanawake Wanasiasa, Dar24 Media ilizungumza na Grace Bruno, yeye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Amani, uliopo kata ya Liwiti, Tabata  jijini Dar es salaam.

Anasema, ‘Wanasiasa Wanawake wengi wanapata msongo wa mawazo na sonona na hali hiyo hudhoofisha na Wanawake wengi kwa ngazi mbalimbali za uongozi, baada ya kufanyiwa ukatili hupoteza ujasiri katika majukwaa ya kisiasa, au pale inapobidi kutoa hoja zake za kisiasa za kusaidia jimbo, kata au jamii husika.”

Aidha, ripoti ya Tech Media Convergence 2021 nayo inaonesha hatua ambazo zilichukuliwa kwa Wanawake wanasiasa baada ya kufanyiwa ukatili mtandaoni kuwa asilimia 3.5 walitoa taarifa kwa mamlaka husika.

Asilimia 41.7 wao waliacha moja kwa moja kutumia mitandao ya kijamii, asilimia 34.9 walipumzika kwa muda kutumia mitandao ya kijamii na asilimia 2.6 walitafuta ushauri wa kisheria uliotumika kuwapa usaidizi.

Japokuwa Wanawake wengi huathirika na ukatili mtandaoni, hali hii imekuwa tofauti kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye yeye, ameonekana kuwa imara na akiendelea na kazi bila kutetereka.

Mapinduzi ya kidigitali, yamepelekea watu kutumia maneno yasiyo na staha mtandaoni dhidi yake, lakini uimara, uhodari, uvumilivu na ustahimilivu wake ni majibu tosha kuwa umemfanya aendeleze malengo yake ya kujenga uchumi wa nchi.

Rais Samia alithibitisha hili alipohutubia katika hafla ya kupokea Gawio na michango kutoka kwa Mashirika mbalimbali na Taasisi za Umma, akisema, “mimi kazi mliyonipa nasimama naifanya, mnayashuhudia matusi ninayotukanwa, mpuuzi hana maana, huyu mbibi eeh eeh, ana hivi, mambo tele lakini najigeuza chura.”

Mama aliongeza kuwa, “kelele nyingi zinapigwa wakiona haujibu wanasema sasa tulitukane litajibu au halijibu, sijibu, ninajigeuza chura masikio sisikii kabisa . Ninachotaka ni mageuzi ya kiuchumi ndani ya nchi anayetaka kunikera mimi anikanyagie uchumi wangu.”

Kauli hii inaonesha jinsi gani Rais Samia alivyo Mwanamke shupavu na hodari asiyetikisika kirahisi na hivyo kuwa mfano, kama kauli mbiu yake isemavyo “Kazi Iendelee” na hivyo yeye kuendeleza mapambano ya kiuchumi na kujenga taifa bila kujali mashambulizi hasi dhidi yake.

Hata hivyo, hapa Rais Samia ameonesha ni jinsi gani amewapa somo “wabonyeza vitufe” hao wasio na fikra chanya kimaadili na kutoa mwanya kwa wenye ueledi kulipambania jambo hili na kutoa elimu kwani si vyema kuzikashifu mamlaka, si vyema kumtamkia Kiongozi Mkuu wa Nchi maneno mabaya na pia si sawa kuwatusi mitandaoni viongozi wote au jamii yenyewe kwa yenyewe bila kujali jinsia.

Hivyo ni muhimu jamii ikapaza sauti kuwa mitandao ya kijamii isiwe cha kuwafanya Wanawake Wanasiasa kuacha kuitumia kwa hofu ya kusemwa isivyo, kwani ina manufaa mbalimbali kwao na pia ni haki yao kimsingi.

Ieleweke kuwa kupitia fursa hiyo, Wanawake wanapata nafasi ya kujipambanua kisiasa, kuushirikishia umma mambo yanayoendelea kwenye kada zao kikazi, kuonesha fursa na utekelezaji wao wa shughuli mbalimbali katika jamii na hata kupata taarifa na wao kujifunza mambo mapya.

Ripoti ya Tech Media Convergence ya mwaka 2021, inaonesha kuwa asilimia 90 wanasiasa Wanawake wamekubali kuwa mitandao inawasaidia kujipambanua kisiasa, hivyo ni jukumu la Taasisi za kielimu na vyombo vya Habari kuhakikisha wanaelimisha na kupigania haki ya Mwanamke ya matumizi ya mitandao ya kijamii yaliyo na staha.

Wasalaam.

Jengo jipya la Halmashauri: Rais ampa maagizo Mkurugenzi
Kalambo: Rais Samia azindua Jengo la Utawala la Halmashauri