Johansen Buberwa – Kagera.
Mradi wa ukarabati na upanuzi wa Bandari ya Bukoba, umesimama kutokana na kukumbwa na changamoto ya mwamba ambao umebainika chini ya maji katika Ziwa Victoria.
Mkandarasi wa Mradi Mhandisi Mnanka Maginga ameyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa mradi huo Julai 16 mwaka 2024 kwa Wajumbe wa kamati ya Kitaifa ya uhamisishaji Biashara Mkoani Kagera.
Amesema mwamba huo wa Granite Rocks wenye ukubwa wa mita 300 chini ya maji umesimamisha ujenzi ambao ulikuwa umefikia asilimia 63 na unahitaji upasuaji wa kina.
“Mradi huo pamoja na miundombinu mingine unajumuisha ujenzi na uboreshaji wa magati matatu pamoja na Jengo la kupokelea abiria zaidi ya 350 katika bandari hiyo ya Bukoba kwa gharama ya zaidi ya Sh.20 Bilioni,” amesema mwandisi Maginga.
Aidha Magiga amesema kuwa Mradi huo unatekelezwa kwa muda wa miezi 20 ulianza kutekelezwa tangu Januari 26 mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika Septemba 09 mwaka 2024.
Mkuu wa Wilaya Bukoba, Erasto Sima kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Hajati Fatma Mwasa akisoma taarifa ya hali ya uchumu wa mkoa Julai 15 mwaka 2024 katika mapokezi ya kamati ya Taifa ya uhamasishaji Biashara, amesema Mkoa huo una fursa nyingi za kiuchumi kutokana na kupakana na nchi nyingi.
Kwa upande Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara Mkoa Kagera, Nicholas Basimaki akizungumza na Dar24 Media amesema ujenzi miradi ya Bandari ya Bukoba na Kemondo usipokamilika kwa wakati utakwamisha shughuli za wafanyabiashara.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Dkt. John Simbachawene ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya uhamisishaji Biashara, amesema Mkandarasi na uongozi wa mamlaka ya bandari utafute ufumbuzi wa kutatua changamoto ya upasuaji mwamba huo ili utekelezaji wa mradi uendelee.