Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amepiga marufuku Watumishi wa Umma kusumbuliwa wakati wa kufuatilia taarifa zao za kiutumishi pale wanapohamia kwenye kituo kipya cha kazi, kwani taarifa zao ni jukumu la Waajiri.
Simbachawene ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mlimo katika Kata ya Lufu, Jimbo la Kibakwe, Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma na kudai kuwa suala la taarifa za Mtumishi ni jukumu la Mwajiri.
Amesema, kitendo cha taarifa za watumishi kutohamishwa kumesababisha Watumishi hao kushindwa kupimwa kwenye mfumo wa e-tendaji kazi kwa vile kunakuwa hakuna taarifa za watumishi hao katika kituo kipya cha kazi na hivyo mwisho wake watumishi kusumbuliwa kufuatilia taarifa za kule walikotoka.
Aidha, Simbachawene pia amemuelekeza Katibu Mkuu- UTUMISHI kushirikiana na Mamlaka zingine zilikokasimiwa madaraka hayo ya kuhamisha Watumishi kuhakikisha Mtumishi pindi anapohama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine asisumbuliwe kuhusu taarifa hizo.