Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene amewataka wananchi wa Kibakwe kuendesha kilimo cha biashara kwa kutumia miundombinu ya umeme iliyopo, huku akiwaahidi kuwaletea mradi mkubwa wa kimkakati wa umwagiliaji.

Simbachawene ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wananchi kwa nyakati tofauti kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Idodoma na Malolo, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, ikiwa ni mwendelezo ziara yake ya kikazi katika Jimbo hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akizungumza leo na watumishi na wananchi wa Kijiji cha Idodoma, Kata ya Rudi iliyopo katika Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi.

Amesema, kitendo cha umeme kufika katika vijiji hivyo kutaleta mapinduzi makubwa ambapo ni muda muafaka sasa wa kuhakikisha umeme huo unatumika kuendesha mashine ya kusukuma maji ya kumwagilia kwenye mashambani.

Simbachawene amesema changamoto kubwa ilikuwa ni kilimo cha umwagiliaji cha kutumia nishati ya dizeli na petroli ambapo ilikuwa ni ngumu kuona tija kutokana na gharama kubwa ya nishati hiyo.

Sehemu ya watumishi na wananchi wa Kijiji cha Malolo, Tarafa ya Rudi iliyopo katika Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Jijini Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, wakati wa ziara yake ya kikazi.

Ameongeza kuwa, umwagiliaji umekuwa duni kutokana na mifereji inayotumika kuwa ni ya kizamani na inachangia upotevu mkubwa wa maji.

“Tunataka mabadiliko makubwa katika jimbo letu, tunatamani kuona umeme tulionao unatupeleka mashambani na sio kuutumia tu kwa ajili ya kuwashia taa pekee majumbani mwetu,” alisema Simbachawene.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akifurahia kuruka kwa pamoja na kikundi cha burudani cha kabila la wamaasai katika Kijiji cha Idodoma wakati wa ziara yake ya kikazi.

Umeme huo utatumika kusukuma maji ya kumwagilia usiku na mchana katika mashamba ya wananchi huku akisema miaka 10 ijayo anaviona vijiji hivyo vikiwa katika viwango vya juu kiuchumi.

Kwa upande wake Mkulima, Aidani Chihoma ametumia fursa hiyo kumshukuru Waziri Simbachawene kwa kupeleka umeme katika vijiji hivyo huku akisema ujio huo wa mradi huo wa umwagiliaji utasaidia kuona tija ya kilimo cha vitunguu na maharagwe.

Kijiji cha Idodoma na Malolo ni miongoni mwa vijiji katika Jimbo la Kibakwe vinavyosifika kwa kustawisha zaidi kilimo cha vitunguu na maharagwe ambapo uhitaji wa mazao hayo umekuwa mkubwa ndani na nje ya nchi.

UVCCM wapokea vifaa vya Kilimo vya Milioni 200
Kenya: Mahakama yabatilisha marufuku ya maandamano