Tume ya Taifa ya Umwagiliaji – NIRC, imefanya Mkutano wa Wadau wa Umwagiliaji kwa Skimu za Mwamkulu na Kabage Mkoani Katavi
Akifungua Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa katavi, Mwanamvua Mrindoko , amewaasa wakulima na wananchi wa kata ya Mwamkulu kutumia fursa ya ukarabati wa miundo mbinu ya umwagiliaji kushiriki katika kilimo ili kuinua kipato chao na kuepuka migogoro isiyo ya lazima, inayoweza kukwamisha juhudi za serikali kuwaletea maendeleo.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa amesisitiza kuhusu nia ya serikali kuendelea kuinua na kuboresha kilimo cha Umwagiliaji nchini,kwa kujenga, kuboresha na kuendeleza Miundo mbinu ya Umwagiliaji kwa lengo la kuboresha kilimo cha Umwagiliaji nchini.
Mndolwa amebainisha kuwa Tume imeshapata dhamana ya kuanza na skimu 2 za Mwamkulu na Kabage, ambapo ujenzi unaendelea vizuri na kwamba Mheshimiwa waziri wa Kilimo anakuja kuweka jiwe la msingi.Mkurugenzi mndolwa pia amesema kuwa Tume inaendelea na ujenzi wa Ghala kubwa la kuhifadhi mazao ili kuhakikisha kuwa wakulima hawauzi mpunga badala yake waweze kuuza mchele.
Mndolwa pia ameongeza kuwa, pamoja na ujenzi huo wa miundo mbinu, Tume pia imeweza kufanya jambo la kijamii, kwa kufanya ukarabati wa nyumba ya mganga na wauguzi wa kituo cha afya cha Mwamkulu pamoja na ukarabati wa jengo la huduma kwa wakinaMama katika kituo hicho
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imewekeza zaidi ya Bilioni 54 katika ukarabati na kuboresha Miundo mbinu ya umwagiliaji katika skimu za Mwamkulu na Kabage ambapo wakulima 2500 watanufaika na kwamba miundo mbinu hiyo itahudumia eneo lenye ukubwa wa hekta 6000 katika kata ya Mwamakulu.
Mkutano huo, umejumuisha wakulima wa kata ya Mwamkulu, wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Makao Makuu na Mkoa wa Katavi, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoka, viongozi wa chama ngazi ya Mkoa na wilaya pamoja na wakuu wa wilaya za mkoa wa Katavi.