Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba amewataka Maafisa Habari wa serikali Mkoani Mwanza kubuni habari mpya za kimkakati zenye kuitangaza miradi ya maendeleo ya serikali badala ya kusubiri matukio.

Makoba ameyasema hayo wakati akizungumza na Maafisa Mawasiliano kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa, Taasisi, Mashirika na Makampuni mbalimbali ya serikali Mkoa wa Mwanza katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Amesema anatamani kuona Maafisa hao wakiwa wabunifu zaidi katika kuhakikisha wanauhabarisha umma kwa namna ambayo sio ya kutegemea habari kutoka kwa viongozi tu bali watumie mbinu mbalimbali ili kuonesha utofauti wa utendaji wa sasa na siku za nyuma.

“Na hapa Mwanza ninajua kuna miradi mbalimbali ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya SGR hivyo tusisubiri ijitokeze dosari ukimbilie kutoa taarifa ya ufafanuzi , ni wakati sasa wa kubadili namna ya utoaji wa taarifa zetu,” amesisitiza Makoba.

Aidha, amesema umekua ni utaratibu wake kukutana na Maafisa Mawasiliano kila mahali aendapo lengo likiwa ni kujitambulisha lakini pia kusikiliza na kuchukua maoni, mawazo na mapendekezo mbalimbali ambayo yatasaidia kuboresha utendaji kazi.

Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana amesema Mkoa wa Mwanza ni Mkoa wa kimkakati kwa kuwa ndio lango kuu kwa kanda ya ziwa na ndio kitovu cha uchumi hivyo Maafisa Habari wanategemewa kwenye uhabarishaji na serikali inawapa ushirikiano mzuri.

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali (RS Mwanza), Paulo Zahoro amesema hali ya uhabarishaji kwa Mkoa wa Mwanza ni nzuri hata kufikia hatua ya kushinda nafasi ya pili na kupata Kikombe na Cheti cha Ushindi kutoka kwa Waziri wa Habari Mhe. Nape Nnauye kwenye Kongamano la Habari lililofanyika jijini Dar es Salaam Juni 2024

Dkt. Biteko: Dira ya Taifa 2050 ni maono ya Nchi
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Julai 20, 2024