Shirika la Umeme Tanzania – TANESCO, Mkoa wa Pwani limefanikiwa kufikisha Umeme katika kisiwa cha Chole kilichopo Wilayani Mafia, ambacho hakijawai kuwekwa Umeme tangu uhuru kwa kuupitisha chini ya Bahari.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati Meneja wa TANESCO mkoa wa Pwani, Eng. Cosmas Mkaka akikagua mradi huo, Mbunge wa Jimbo la Mafia ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amshukururu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa fedha za kukamilisha mradi huo.
Amesema huduma hiyo ya umeme katika kisiwa hicho utarahisisha shughuli za Maendeleo kwa Wananchi wa Wilaya ya Mafia.
Naye Meneja wa TANESCO Mkoa wa Pwani, Mkaka amesema mkakati wa TANESCO ni kufikisha Umeme katika visiwa vingine viwili vya Jibondo na Juwani ili kukamilisha uwekaji wa Umeme katika vijiji vyote 23 wilayani Mafia kabla ya kufikia mwaka 2025.
Alisema urefu wa nyaya za Umeme za mradi huo ni mita 1170 utanufaisha kaya zaidi ya 1000 na mradi huo wa Umeme katika visiwa hivyo vidogo vya kisiwa cha Mafia mkoani Pwani kwa gharama ya bilioni 3.2.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Juma Salum amesema kufika Umeme katika visiwa hivyo ni faraja kubwa kwa Wananchi.