Naibu waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Ndariananga amezindua nyaraka za usimamizi wa maafa wilaya ya Kibiti kwa lengo la kusimamia na kuratibu shughuli za kuzuia na kukabiliana na majanga nchini.
Akizungumza Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani amesema moja ya majukumu ya Idara ya Menejimenti ya Maafa kupitia Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 6 ya Mwaka 2022 ni kutayarisha, kuhuisha na kuratibu utekelezaji wa sera, mipango, sheria, kanuni, mikakati na taratibu za utendaji kwenye shughuli zote zinazohusiana na usimamizi wa maafa Tanzania Bara.
Amesema, mpango wa serikali ni kukabiliana na maafa nchi mzima , lakini imeanza na wilaya kibiti kwa kushirikiana na UNDP ili kuweza kujikinga na maafa, huku akikaribisha wadau mbalimbali katika kushirikiana na serikali ili kuweza kufikia malengo.
Ndariananga ameongeza kuwa nyaraka ambazo zimezinduliwa ziende zikatumike katika kutendea kazi kikamilifu huku akisisitiza kuwa kazi imeanza mara baada ya uzinduzi huo na kazi ya uandaaji wa mpango wa kujiandaa na kukabiliana na maafa na Mkakati wa Kupunguza Viatarishi vya Maafa kwa Wilaya ya Kibiti ni muendelezo wa utekelezaji wa jukumu hilo la msingi la Ofisi ya Waziri Mkuu ambalo limelenga kuimarisha usimamizi na uratibu wa Maafa katika ngazi za Mikoa na Wilaya.
“Kama mnavyofahamu katika kipindi cha mwezi Januari hadi Mei, 2024 mvua kubwa zilizonyesha katika maeneo mbalimbali Nchini na kusababisha Maafa ya Mafuriko katika maeneo mengi ikiwemo Mkoa wa Pwani Mafuriko haya yalisababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa mali, miundombinu na mazingira,” alisema Ummy.
Aliongezea kuwa kufuatia hali hiyo Serikali kwa kushirikiana na wadau ilichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuratibu upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa waathirika, kuimarisha huduma za Afya, kutoa huduma ya Afya ya akili na msaada wa kisaikolojia na kijamii, kuratibu na kutekeleza operesheni ya utafutaji na uokoaji, kutafuta, kukusanya na kugawa misaada ya kibinadamu na kurejesha miundombinu iliyoathirika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Brig. General Hosea Ndagala, amesema kuwa wanaendelea kuimarisha utekelezaji katika ngazi ya wilaya kupitia mafunzo yanayotolewa.
Naye mtaalam wa miradi UNDP Abbas Kitogo amesema kuwa nyaraka hizo ni chachu kwa jamii katika kukabiriana na majanga mbalimbali, huku akisisitiza kuwa UNDP itaendelea kushirikiana na serikali katika kupambana na majanga.
UNDP imepokea shilingi Billion 23 kwa ajili ya kukabiliana na maafa kwa kushirikiana na mamlaka ya Hali ya Hewa TMA.