Bunge la India limeahidi kutoa fursa zaidi za mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi wa umma kupitia Taasisi yake ya Utafiti na Mafunzo ya Kidemokrasia (PRIDE) inayoendeshwa na Bunge hilo.
Ahadi hiyo imetolewa na Spika wa Bunge la India (Lok Sabha), Mhe. Om Birla wakati wa mazungumzo yake na Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson katika Ofisi za Bunge hilo Jijini New Delhi.
Katika mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine, Birla amemuelezea Dkt. Tulia kuhusu maboresho yaliyofanywa na Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya ufadhili kwa Watumishi wa umma kutoka nchini mbalimbali Duniani hususani Wabunge na Watumishi wa Mabunge ya nchi hizo.
Vilevile, Birla ametoa kipaumbele mahususi kwa Watumishi wa Tanzania kwa kuzingatia urafiki, historia na uhusiano uliodumu kwa muda mrefu baina ya Tanzania na India. Aidha, kwa kutambua pia nafasi ya Dkt. Tulia kuwa Rais wa IPU, ameahidi kupitia PRIDE kushirikiana na IPU kuandaa mafunzo kwa Watumishi na Wabunge Wanachama wa Umoja huo.
Aidha, Dkt. Tulia ametumia fursa hiyo kulishukuru Bunge la India kwa kumuunga mkono wakati wa kampeni za Uchaguzi wa Urais wa IPU pamoja na Bunge hilo kuendelea kusimamia misingi ya demokrasia, utawala bora na kuongeza idadi ya Wabunge wanawake na makundi maalum katika Bunge hilo.