Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ametatua mgogoro baina ya Wachimbaji Wadogo na Mwekezaji Kampuni ya Uchimbaji wa Kati ya Canuck Co. Limited inayomiliki Leseni ya Uchimbaji wa Kati (ML) katika Kata ya Mwakata, Halmashauri ya Msalala, Wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga.
Hayo yamejiri, Julai 26, 2024, mjini Kahama, wakati wa kikao baina ya Naibu Waziri, Mwekezaji huyo, Wamiliki wa ardhi na Wachimbaji hao waliokuwa wanafanya shughuli za uchimbaji zisizo rasmi kinyume na Sheria ya Madini katika eneo hilo lililopo Kitongoji cha Magunh’umwa, Kata ya Mwakata katika Halmashauri hiyo.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, maamuzi ya kikao hicho ni utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa katika ziara yake ya tarehe 22 Februari, 2024, kuhusu mgogoro huo ambapo alitoa kipindi cha miezi mitatu kwa pande hizo mbili kukaa na kujadiliana namna bora ya kutatua changamoto hiyo kwa kutumia busara.
Hata hivyo, baada ya kumalizika kwa kipindi hicho, hakuna hatua yoyote iliyofikiwa baina ya pande hizo mbili na kwamba utaratibu unapaswa kufuatwa.
Kupitia kikao hicho, Dkt. Kiruswa ameagiza kusitishwa kwa shughuli za uchimbaji katika eneo hilo kuanzia leo (Julai 26, 2024) na kutoa siku saba kwa wachimbaji hao kuondoa vifaa vyao vilivyokuwa vinatumika eneo hilo. Pia, ameitaka Tume ya Madini kuhakikisha mipasuko inazibwa na kuweka mageti.
Aidha, Dkt. Kiruswa ameiagiza Halmashauri ya Msalala kuhakikisha inawafanyia tathmini wananchi 23 wanaomiliki ardhi katika eneo hilo ili walipwe fidia na mwekezaji huyo na hatimaye kupisha mradi na kumtaka mwekezaji huyo kuhakikisha anaendana na leseni ya uchimbaji wa kati kwa kutumia teknolojia inayokubalika kisheria.
Aidha, Dkt. Kiruswa ameilekeza Tume ya Madini kutoa maeneo na leseni kwa wachimbaji wadogo waliopisha miradi ya uwekezaji ili kuwarasimisha huku akiitaka Tume ya Madini, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Halmashauri hiyo, na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu umuhimu wa kumiliki leseni na zoezi la uthaminishaji wa ardhi.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Kahama, Winnifrida Mrema, amesema kuwa Ofisi ya Tume ya Madini katika Mkoa huo wa kimadini iko tayari kutoa maeneo mengine inayoshikilia leseni na kuwapatia wachimbaji hao waliopisha mradi huo ili kuwapa fursa ya kuendelea kuchimba na kujipatia kipato sambamba na kuendesha maisha yao.
Kikao hicho, pia, kimehudhuriwa na Katibu Tawala Wilaya ya Kahama Hamad Mbega akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, Khamis Katimba, pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Dhahabu Mkoa wa Shinyanga (SHIREMA), Hamza Tandiko.