Naibu Katibu Mkuu Elimu OR TAMISEMI, Dkt. Charles Msonde amesema kuwa, upatikanaji wa madarasa janja (smart classrooms) utasaidia kwa kiwango kikubwa katika kuongeza ufanisi wa ujifunzaji na ufundishaji nchini pamoja na kupunguza changamoto ya upungufu wa walimu.

Dkt. Msonde amesema hayo hivi karibuni katika ofisi za Taasisi ya Elimu Tanzania Jijini Dar es Salaam kwenye hafla fupi iliyowakutanisha viongozi kutoka Shanghai na Tanzania ambao pamoja na kujadiliana masuala mbalimbali ya uboreshaji wa elimu, walijionea utendaji kazi wa madarasa janja yaliyounganishwa kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Dodoma, Pwani na Zanzibar.

Amesema kuwa katika kipindi hiki cha utekelezaji wa mafunzo ya Mtaala ulioboreshwa matumizi ya teknolojia ya darasa janja hayaepukiki na yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuwafikia walimu wengi nchi nzima.

Sambamba na hilo, amewashukuru Wakurugenzi kutoka Shanghai, Taasisi ya Elimu Tanzania pamoja na Kampuni ya EduTech kwa kuunganisha jitihada kwa pamoja katika upatikanaji wa madarasa janja yatakayosaidia katika utoaji wa mafunzo katika maeneo mengi kwa wakati mmoja.

Aidha, Dkt. Msonde amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa Elimu nchini, Serikali kupitia OR-TAMISEMI imeelekeza halmashauri zote nchini kuhakikisha zina darasa janja moja mpaka matatu kadiri ya mahitaji yao, na kusisitiza kila Mkoa unapaswa kuwa na darasa janja moja ili kuzilisha shule zilizo kwenye halmashauri.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi kutoka Wizara ya Elimu Tanzania, OR TAMISEMI, Mkurugenzi wa Elimu China, Viongozi wa TET, Walimu kutoka chuo Kikuu cha Shanghai, TET, shule za Olimpio, Diamond, Zanaki na Tambaza.

Katimba: Simamieni miradi ya elimu kwa weledi
Marufuku uchomaji taka kwenye Hifadhi ya Bahari - NEMC