Jeshi na idara ya usalama DSS nchini Nigeria, wametoa onyo kwa Waandamanaji kutofanya ghasia mfanano na za Kenya, katika maandamano yaliyopangwa kufanyika wiki ijayo ya kupinga kupanda kwa gharama za maisha.
Hatua hiyo inafuatia hamasa ya mtandaoni I ayowataka Wanigeria kuingia mitaani kuanzia Agosti 1, 2024 kuandamana, huku ikiwa haijulikani ni nani anahusika na uratibu wa maandamano hayo huku watu wengi wao wakiwa na wasiwasi wa kupoteza ajira zao na wakichukua tahadhari ya ukandamizwaji uliopitiliza.
Wito huo, nunakuja kipindi hiki ambacho Wanigeria wengi wanapambana na ukali wa maisha, baada ya Rais wao, Bola Ahmed Tinubu kusitisha mpango wenye gharama kubwa wa ruzuku ya mafuta na kuondoka vikwazo vya ubadilishanaji wa sarafu ya naira, ili kufufua uchumi wa taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika.
Nigeria limeshuhudia vurugu ndogo kuhusiana na mageuzi yake ya kiuchumi ambayo tayari yamesababisha ongezeko la asilimia 40 la mfumuko wa bei za chakula, hivyo onyo hilo limeakisi kilichotokea Kenya iliyokumbwa na maandamano ya maafa, yalioilaazimu Serikali kuachana na mpango wa kuongeza kodi.