Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema mpaka sasa mradi wa ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa Masoko imeshatoa ajira kwa vijana wapatao 570 ambao wanafanyakazi hapo huku akiongeza kuwa utakapo kamilika utatoa ajira elfu 30 katika nyanja mbalimbali.

Waziri Ulega amesema hayo leo alipotembelea kukagua maendelea ya ujenzi wa mradi huo unaofanyika wilayani Kilwa, mkoani Lindi Julai 30, 2024.

“Leo nimekuja kutembelea huu mradi nimewakuta vijana wanafurahia kazi wanayoifanya. Vijana wa taifa zima watapata fursa ya kufanya, tunataraji vijana wasiopungua elfu 30 kutoka maeneo mbalimbali watapata ajira hapa, Tunamshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu ambao ni wa kilelezo kwa taifa letu,” amesema.

Wakati huohuo: Waziri Ulega amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ambao mpaka sasa umefikia asilimia 63 na unatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2025.

Amesema bandari hiyo ya uvuvi inayojengwa kwa fedha za ndani ni mradi wa kielelezo unaotekelezwa chini ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Mradi huu tuutazame kama mboni ya jicho letu ili uwe endelevu kwa maana ukikamilika utainua uchumi wa Kilwa, ukanda wa Kusini na Taifa kwa ujumla”, amesema.

“Nimefurahi hatua ni nzuri, tumepiga hatua zaidi ya nusu, muhimu kuhakikisha kazi inakwisha kwa wakati ili Watanzania waweze kuona thamani ya pesa zao, shukrani nyingi kwa rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuujenga mradi huu ambao ni wa kielelezo kwa taifa letu,” alifafanua.

Kabuje: Watoto wanaoishi mazingira hatarishi wasaidiwe
Kilombero: Wakulima wa Miwa wampinga Mpina