Watumishi wa Serikali watakaofanya ununuzi wa Umma nje ya Mfumo wa NeST watakuwa wamefanya kosa la jinai, na kukabiliwa na adhabu ya kifungo jela pamoja na kulipa faini, kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023.
Akizungumza kwenye kipindi maalum cha Tenda Radio, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Wakili Paul Kadushi, amewataka viongozi wa taasisi za serikali na watumishi kwa ujumla kuzingatia matakwa ya sheria hiyo iliyoanza kutumika Juni 17, 2024 na kanuni zake ambazo zimeanza kutumika Julai 1, 2024.
Kadushi amefafanua kuwa sheria iliyofutwa haikuweka ulazima wa kutumia mfumo wa kielektroniki kufanya ununuzi, hatua iliyosababisha taasisi nyingi kufanya ununuzi nje ya mfumo.
“Lakini kwa sheria hii mpya [Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023] sasa imeweka sharti la lazima kwa taasisi nunuzi zote kutumia mfumo wa kielektroniki katika kufanya ununuzi,” Wakili Kadushi aliiambia Tenda Radio.
“Na kwa mtumishi wa umma atakayekiuka matakwa haya ya sheria, Kifungu cha 128 (2) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 kimeweka bayana kwamba atakuwa ametenda kosa la jinai na akitiwa hatiani atakabiliwa na adhabu ya kifungo jela kisichozidi miaka mitatu au kulipa faini isiyozidi shilingi milioni 10 au vyote kwa pamoja,” amesema Kadushi.
Mkurugenzi huyo wa Huduma za Sheria ameeleza kuwa taasisi nunuzi zinapopata changamoto yoyote katika kutumia Mfumo wa NeST zinapaswa kuwasiliana na PPRA ili kupatiwa ufumbuzi.
Amesema PPRA ina Ofisi sita za Kanda ambazo zinatoa huduma kwa wadau wote, pamoja na Ofisi za Makao Makuu zilizoko jijini Dodoma.
Ofisi hizo za Kanda na maeneo ambapo zipo ni Kanda ya Ziwa (Mwanza – Ofisi ya Mkuu wa Mkoa), Kanda ya Kati na Magharibi (Tabora – Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa), Kanda ya Kaskazini (Arusha – Jengo la PSSSF), Kanda ya Pwani (Dar es Salaam – Jengo la Hazina, Mtaa wa Madaraka), Kanda Kusini (Mtwara – Jengo la PSSSF) na Nyanda za Juu Kusini (Mbeya – Jengo la NHIF).
Aidha, amesema kuwa ili kuhakikisha kuwa taasisi zote zina uelewa wa kutumia Mfumo wa NeST, PPRA ilishawapa mafunzo watumishi wa taasisi za umma na inaendelea kutoa mafunzo hayo mara kwa mara. Mafunzo hayo hutolewa pia kwa wazabuni katika mikoa mbalimbali ili wapate fursa ya kushiriki michakato ya ununuzi wa umma kwa uwazi na haki.
Akizungumzia ufanisi wa Mfumo wa NeST, alisema kuwa mfumo huo ambao ulianza kutumika Julai 1, 2023 umeongeza uwazi, uwajibikaji, ushindani wa haki na upatikanaji wa taarifa sahihi.