Boniface Gideon, Mkinga – Tanga.
Zaidi ya Wanufaika 4422 wa mfuko wa Kutunza Bahari ‘MKUBA’ unaodhaminiwa na Shirika la Maendeleo Nchini Norway ‘NORAD’,chini ya usimamizi wa Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania ,wametakiwa kudumisha nidhamu ya matumizi ya Fedha na kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuwainua kiuchumi pamoja na kuwa mabalozi wa kutoa Elimu ya utunzaji wa rasilimali za Bahari.
Rai hiyo imetolewa na Ofisa Uvuvi Wilaya ya Mkinga Ezra Katete wakati akikabidhi fedha zaidi ya 31.5 Mil kwa Wanachama wa vikundi vya mkuba kutoka Vijiji vya Zingibari,Moa na Mwaboza vyenye Wanachama zaidi ya 461,
Amesema fedha hizo zitasaidia kuongeza mitaji yakuendesha Biashara zao,hivyo ni vyema nidhamu ya matumizi ya Fedha ikadumishwa.
“tunataka tuone matokeo chanya baada ya muda mfupi ujao,msije mkazitumia kwenye anasa ikiwemo harusi,kulewa na kununulia nguo mnaita vijora na madera,wahisani wetu wanazitoa ili mjikwamue kiuchumi, wahisani wetu wanataka wawawezeshe ili mnapotekeleza majukumu yenu msiwe na changamoto,” ameongeza Katete.
Kwa upande wake mratibu wa miradi kutoka Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania Abubakar Masoud,amesema Vijiji hivyo ni sehemu ya Vijiji 12 vilivyopo wilayani Mkinga na inajumuisha sehemu ya Vijiji 29 vikiwa na vikundi 148 ambavyo vipo kwenye Mradi huo kutoka Halmshauri za Mkinga,Tanga Jiji,Muheza na Pangani ambapo mpaka sasa Vijiji 23 vimeshanufaika na Fedha za Mradi huo,
“fedha hizi tunazokabidhi katika vikundi vya mkuba kwenye Vijiji vya Zingibari, Moa na Mwaboza ni mwendelezo wetu wa kuwafikia Wakazi wanaoishi Mwambao wa Bahari,tumewapatia Elimu ya utunzaji wa rasilimali za Bahari na Usimamizi wa Fedha, lakini pia tunawawezesha kiuchumi ili wasiwe na njaa wanapotekeleza majukumu yao,” ameongeza Masoud.
Kwa upande wake Msimamizi Mratibu wa Shirika hilo Mkoa wa Tanga, Ahmad Salim Omar amesema juhudi za ziada zinahitajika kunusuru rasilimali za Bahari kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu.
Amesema, “kutokana na kuongezeka kwa watu,hali hii imepelekea kuongezeka kwa shughuli nyingi za kibinadamu Baharini,ukataji wa miti aina ya mikoko,uvuvi haramu wa kutumia Baruti na sumu lakini pia uchafuzi wa fukwe za Bahari.”
“Hivyo baada yakuona hivyo tuliamua kuja na miradi ikiwemo ‘MKUBA’,ambapo tunalenga kuwawezesha kiuchumi Wanachama wa vikundi lakini pia tunatoa Elimu ya utunzaji wa rasilimali za Bahari ikiwemo upandaji wa mikoko na usafi wa fukwe uvuvi.” aliongeza Ahmad.