Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ametoa wito kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika kuridhia Itifaki ya Uhuru wa Watu Kusafiri bila Vikwazo ili kurahisisha ufanyaji biashara baina ya nchi hizo kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Balozi Mussa ametoa wito huo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Majadiliano kuhusu Fursa na Changamoto za Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika kuhusu Uhuru wa Watu Kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo na uzoefu kutoka Jumuiya za Kikanda na Umoja wa Ulaya uliofanyika mjini Unguja, Zanzibar.

Amesema kuwa faida za Itifaki hiyo ni nyingi kwa watu wa Afrika ambapo mbali na kurahisisha usafiri wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine na ni muhimu katika ukuzaji rasilimali watu na kutengeneza fursa kwa vijana kama vile biashara, utalii, kuimarisha utamaduni miongoni mwa watu na kwa kiasi kikubwa itakuza uchumi wa nchi za Afrika. Itifaki hiyo pia itawawezesha raia kutoka nchi za Afrika kuishi na kujenga uchumi kwa maendeleo endelevu ya Bara la Afrika.

Amesema mafanikio ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) ambao umeanza kutekelezwa na nchi wanachama tangu mwaka 2021, yatafikiwa kikamilifu pale nchi zote wanachama zitakaporidhia Itifaki hii ili kwenda sambamba na Itifaki nyingine za Uhuru wa Kuingiza Bidhaa na Uhuru wa Kutoa Huduma.

“Ninafurahi kwamba Nchi nyingi na Jumuiya za Kikanda za Kiuchumi kama EAC, ECOWAS, IGAD na SADC zimefanyia kazi Itifaki hii kupitia kanda zao na lengo ni kuongeza zaidi uhuru wa watu wa Afrika kutembea kutoka nchi moja kwenda nyingine,” amesema Balozi Mussa.

Pia amewataka wajumbe wa mkutano huo kujadili changamoto mbalimbali zinazokwamisha kuridhiwa kwa Itifaki hiyo ambayo ilipitishwa na nchi za Afrika mwaka 2018 ambapo hadi sasa ni nchi nne pekee zimeridhia itifaki hiyo inayohitaji nchi 15 kuiridhia ili kuanza utekelezaji wake.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Balozi na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Afrika, Innocent Shiyo amesema kuwa Mkutano huo utajikita katika kuainisha changamoto na nini kifanyike ili kuwezesha kuridhiwa na kuanza kutumika kwa Itifaki hiyo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Bara la Afrika hususan katika sekta ya ukuzaji biashara, utalii na uchumi kwa ujumla. Pia amesema wajumbe watajadili, kujifunza na kubadilishana uzoefu kutoka Jumuiya za Kikanda na nchi ambazo tayari zimeridhia Itifaki hiyo.

Naye Mkuu wa Idara ya masuala ya Kibinadamu na Harakati Huru kutoka AIJC, Rita Amijkhobu amesema Itifaki hiyo ikianza kutumika itainganisha Afrika na kuwa kitu kimoja ambapo itawezesha watu kupita kwenye mipaka kwenda nchi nyingine bila vikwazo hatua itakayosaidia mzunguko wa biashara kukua kwa haraka.

Tetesi za Usajili Duniani leo Ijumaa tarehe 02 agosti 2024
Wanachama wa MKUBA wakumbushwa nidhamu ya fedha