Lydia Mollel – Morogoro.

Maendeleo ya wananchi yamekuwa yakitegemea sana uchaguzi bora wa viongozi wenye nia thabiti ya kuleta mabadiliko,viongozi walio na malengo ya kuwasaidia wananchi kuondokana na umasikini kwa kuhamasisha na kuboresha huduma muhimu, kama vile kilimo, uvuvi, na ufugaji wa kisasa, hususan viongozi wa mitaa.

Hayo yamesemwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge alipotembelea banda la Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika Mkoani Morogoro yanayo unganisha mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es salaam na Morogoro.

Meya ameongeza kuwa, wananchi wanapaswa kufahamu umuhimu wa kuchagua viongozi wenye maadili na uwezo wa kusukuma mbele ajenda za kimaendeleo na sio wale wanaojali maslai yao binafsi.

“Kama mnavyofahamu mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa,na sisi tunasema maendeleo ya kwanza yanaanzia kwa viongozi wanaishi na wananchi,ambao ni wakulima,wafugaji,wafanyabiashara na wavuvi wanaishi katika mitaa yetu,ukizingatia kauli mbiu ya uchaguzi mwaka huu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.”

“Hivyo nitoe wito kwa wananchi kuchagua viongozi bora kwani watawasaidia kuboresha yote hayo,sisi tunataka watu wafuge vizuri,walime kilimo cha kisasa lakini pia wafanyabiashara kwa weledi kwa pamoja tupate maendeleo ” Alisema Mnyonge.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Hanifa Hamza amesema licha ya uchaguzi wa viongozi bora utakaofanywa na wananchi,lakini wanapaswa kuondokana na dhana ya kuwa kilimo inahitaji maeneo makubwa na kujifunza  kutumia kilimo cha kisasa mjini, hata kama wanayo maeneo madogo ya kilimo.

“Kama mnavyojua Katika Manispaa yetu ya Kinondoni hakuna mashamba makubwa na maeneo karibu yote ni mji,lakini  tunataka kila mmoja aondokane na dhana ya kwamba unahitaji eneo kubwa kulima, ukiangalia hapa tunashughuli zilizofanyika za kilimo,sisi tunataka kuonyesha kuwa inawezekana kulima kisasa na kupata mavuno mengi hata kama eneo lako ni  dogo, unaweza ukaishi  juu gorofani lakini ukalima ,sio lazima kuwa na shamba au eneo kubwa ndo ujishughulishe na kilimo,unaweza kuchukua makopo yako ukaotesha ukavuna,” alisema Hanifa

Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa kwa kutumia teknolojia za kisasa na mbinu bora za kilimo, hivyo wananchi wajitokeze kujifunza njia mpya ya kilimo cha kisasa pamoja na kupata ushauri kwa wataalamu mbalimbali wa kilimo na mifugo.

Nusrat Shafiq Mkazi wa Morogoro, amesema amepata nafasi ya kuona na kujifunza kuhusu mbinu za kilimo cha kisasa, ufugaji bora, na uvuvi, ambazo zinaweza kumsaidia kuongeza kipato kwani amepata elimu mpya.

“Nilikuwa nasikia kilimo cha kisasa,nikawa nafikiri ni mambo ya mbolea na mashine za kumwagilia, lakini leo nilivyokuja hapa kwenye maonyesho nimekutana na kitu cha tofauti hapa Kinondoni,kweli nimejifunza kuanzisha busting inawezekana hata kwenye ndoo nyumbani, na mimi nitaenda kujaribu lakini pia wametupa elimu namna ya kufanya na kutunza mmeo ili uweze kuvuna bila changamoto yoyote”Alisema Shafiq.

Boniface Lymo ambae pia ni Mkazi wa Morogoro, amesema kuwa amejifunza mbinu za ufugaji wa kisasa katika kutunza afya ya mifugo, kulisha kwa kutumia chakula bora na mbinu za kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama na pia anaamini kuwa mafunzo haya yatamsaidia kuboresha ufugaji wake na kuongeza kipato cha familia yake.

“Haiitaji wanyama wengi kutengeza faidi nilichokiona hapa unahitaji huduma bora kwenye mifugo yako,hatakama wakiwa wawili wanatosha kuzalisha faida,mfano kwa wafugaji wa ng’ombe lishe bora inatosha kukuzalishia maziwa mengi sana kwa mfugo mmoja sio lazima wawe wengi,elimu niliyoipata hapa nitaitumia kwanza itanirahisihia kutunza mazingira na kuepukana na migogoro isiyo yalazima,lakini pia nitapata fedha ya kujikimu na familia yangu,” alisema Lymo.

Katika maonyesho ya Nanenane  Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeonyesha mikakati yake ya kuwasaidia wakulima wadogo wadogo na kuhakikisha kuwa wanapata mbegu bora, mbolea, na elimu ya kutosha ili kuhakikisha kila mmoja anajikwamua kiuchumi.

Mchengerwa: Daraja la Berega kuwakomboa Wananchi
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Agosti 3, 2024