Kufuatia vifo vya takribani watu 13 waliofariki Agosti 1, 2024 wakati wa maandamano ya kupinga utawala mbaya na kupanda kwa gharama ya maisha nchini Nigeria, Jeshi la Polisi limetupiwa lawama kwa matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Lawama hizo zimetolewa na Shirika lisilo la kiserikali la Amnesty International, ambalo linashutumu polisi kuwaua raia hao waliokuwa wakiandamana kwa amani, huku Polisi wakijitetea bila kutoa maelezo zaidi kuwa watu wanne kati ya hao waliuawa katika milipuko.
Amnesty kupitia chapisho lake la mtandao wa X limearifu kuwa Watu sita waliuawa katika mji wa Suleja uliopo karibu na mji mkuu Abuja na wengine wanne waliuawa huko Maiduguri kaskazini-mashariki mwa Nigeria huku watatu wakipoteza maisha huko Kaduna eneo lilipo kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
“Ushahidi wetu, katika hatua hii, unaonyesha kwamba pale palipokuwa na vifo, askari wa usalama walitumia mbinu za makusudi kuua wakati wakikabiliana na mikusanyiko ya watu wanaokemea njaa na umaskini mkubwa,” wameandika Amnesty.
Mapema hapo Agosti 2, 2024 mjini Abuja, Polisi walifyatua vilipuzi vya kutoa machozi kwa makumi ya waandamanaji waliokuwa wakishiriki katika siku ya pili ya maandamano hayo ya kupinga utawala mbovu na kupanda kwa gharama za maisha.