Wananchi wa Kijiji cha Ngomai kilichopo Wilayani Kongwa mkoani Dodoma wamefanya harambee ya kumpongeza muuguzi wa kijiji hicho, Peter Mwakalosi kwa kufanya kazi kwa moyo wa ukarimu, upendo, kujitoa na kuzingatia maadili ya taaluma yake.
Harambee hiyo ilifanyika kijijini hapo kwa Wananchi hao kuchanga zaidi ya Shilingi milioni nne, kwa ajili ya kumnunulia kiwanja muuguzi huyo ili aweze kujenga na kuishi kijijini hapo hata atakapostaafu kazi.
Mgeni rasmi katika harambee hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kongwa, Dkt. Omary Nkullo amesema Wananchi hao wameonesha moyo wa shukrani na jambo la kuigwa na watu wengine.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ngomai, Mfaume Mlimila amemuomba mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kongwa asimhamishe muuguzi huyo kijijini hapo kwani anafanya kazi kubwa ya kutoa huduma nzuri ya afya.