Lydia Mollel – Morogoro.

Rais Samia Suluhu Hassan amezindua jengo mtambuka lenye mahabara pamoja na madarasa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), iliyogharimu shilingi bilioni 11.4 jengo hilo lina uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 3,200, itasaidia kuboresha elimu ya vitendo kwa wanafunzi wa programu mbalimbali.

Hayo yamejiri katika uzinduzi wa jengo hilo uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mjini Morogoro.

Akizungumza na Dar24 Media, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Raphael Chibunda amesema  jengo hilo limejengewa fedha kutoka serikali kuu pamoja na fedha za ndani ya chuo na lina uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 3,200, ambapo kila maabara inaweza kuhudumia wanafunzi 150 kwa awamu moja.

“Jengo hili limegarimu Billioni 11.4,fedha hizo ni fedha kutoka serikali kuu pamoja na fedha zetu za ndani ya chuo na ina  manufaa makubwa kwa sababu tulikuwa na uhaba mkubwa wa madarasa ya kufundishia, pamoja na maabara za kufundishia kwa vitendo wanafunzi wetu wa programu mbalimbali.

Jengo hili lina ukubwa wa kuchukua wanafunzi 3,230, lina maabara nane kubwa ambazo zina uwezo wa kuchukua wanafunzi 150 kila moja vilevile, tuna madarasa makubwa nane ambayo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi kwa idadi tofauti tofauti namshukuru Mh. Rais kwa kutembelea chuo chetu na mambo makubwa anayoendelea kuifanyia nchi yetu,” aliongeza.

 

Chibunda ameongeza kuwa Maabara hiyo mpya inatarajiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya kujifunzia kwa vitendo, hivyo kuongeza ubora wa elimu inayotolewa kwa wanafunzi wa SUA na kuchangia maendeleo ya kitaaluma nchini.

“Kati ya mambo muhimu na ya kipekee ambayo Rais Samia amefanya ni kuzindua jengo la maabara yetu kubwa (jengo mtambuka,wakati alipokuwa Makamu wa Rais wa nchi yetu, alikuja kuweka jiwe la msingi na leo amelizindua ni heshima kubwa sana,”

“Jengo hili lilianza kujengwa kipindi cha awamu ya tano na sasa ina miaka mitano hadi kukamilika kwakwe, lakini tunashukuru sana serikali ya awamu ya sita kwa fedha ambazo zimeendelea kutolewa ili kumalizia jengo hili,kwani kutaongeza chachu ya kujifunzia na pia tutazalisha wataalamu wengi nchini waliobebea kwa vitendo,” alisema Prof. Chibunda.

Amina Juma, mwanafunzi wa mwaka wa pili katika kitivo cha Kilimo, amesema Uwepo maabara ya kisasa ni fursa kwa wanafunzi kujifunza kwa upana zaidi.

“Uwepo wa maabara hii utatusaidia sana sisi kama wanafunzi kutapata fursa ya kujifunza kwa vitendo zaidi na kuimarisha maarifa yetu kwa njia ya kisayansi,hii ni fursa kubwa sana kwetu,sisi tumekuwa tukifanya vizuri miaka yote lakini hii itakuwa chachu ya kufanya vizuri zaidi na kutupa moyo wa kuona kuwa tunadhaminiwa na kujaliwa kwenye kile ambacho tunakifanya kwa sasa,” alisema Amina.

James Mwakalinga, Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa kitivo cha Sayansi ya Wanyama, amesema Maabara hiyo itaboresha ufanisi wa tafiti zitakazofanyika chuoni hapa kwani kwa sasa wana vifaa vya kisasa visivyo na mashaka yoyote.

“Maabara hii itatupa nafasi ya kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitasaidia kuboresha mbinu za kilimo na ufugaji hapa nchini,tutaweza kufanya majaribio kwa vitendo na kujifunza kwa undani zaidi,kwa sasa atuna hofu ya kupatia au kukosea tuna vifaa vya kisasa vya kufanyia tafiti mahabara kubwa na yenye nafasi za kutosha,” alisema Mwakalinga.

Hata hivyo , Rais Samia aliridhia jengo hilo kupewa jina la Samia Suluhu Hassan Teaching Complex huku Wanafunzi wa SUA wakiwa na matumaini makubwa kwamba maabara hiyo itachangia kuongeza ujuzi na maarifa yao, kwa kuwaandaa vyema kwa ajili ya soko la ajira na utafiti, wakiamini kuwa uwekezaji huo ni hatua kubwa kuelekea maendeleo endelevu ya sekta ya elimu na sayansi nchini.

Mashabiki nane wa soka kutembelea Dubai
Usimamizi wa Miradi: Wizara ya Nishati iongeze kasi - Rais Samia