Johansen Buberwa – Kagera.
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imefanikuwa kuokoa kiasi cha fedha zaidi ya shilingi milioni 4.3 za wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya umasikini TASAF 139 katika Wilaya ya Ngara.
Akizungumza na vyombo vya Habari ofisini kwake, Naibu Mkuu wa TAKUKURU, Ezekia Sinkala amesema katika kipindi ch Machi – Juni Taasisi hiyo ilifanikiwa kuokoa kiasi hicho cha fedha baada ya kupokea taarifa ya ubadhilifu kwenye kijiji cha Kumutana kilichopo Kata ya Kibimba, Wilayani Ngara.
Amesema, baada ya kufanyika uchunguzi ilibainika mnamo mwezi Septemba 24 mwaka 2020 kulikuwa na zoezi la uhalalishaji wa fedha za Tasaf katika kijiji hicho za kipindi cha mwezi mei hadi juni na mwezi julai hadi Agosti yaani mgao wa madirisha mawili kwa wanufaika.
“Katika ufatiliaji ilibainika kwamba fedha husika zilizochukuliwa na kupelekwa kijiji cha kumutana zilikuwa jumla ya shilingi milioni 9,332,000 kwa awamu zote mbili yani kiasi cha shilingi milioni 4,666,000 kwa kila awamu lakini kwa makusudi wasimamizi walitumia uelewa mdogo wa wanufaika na kuwalipa fedha ya awamu moja badala ya mbili,” alisema Sinkala.
Ameongeza kuwa, mwaka 2021 wasimamizi walirejesha sehemu ya fedha kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngara iliyorejeshwa kwa Wananchi ambapo wasimamizi husika walishindwa kurejesha kiasi cha fedha kilichobaki na kukana kuhusika na ubadhirifu huo hadi ulipofanyika uchunguzi na kuthibitika kuwa ni kweli walilipa awamu moja badala ya mbili.
Kwa upande wao Wanakijii cha Kumtana wameishukuru TAKUKURU na Serikali kwa kwa kufanikisha kurejeshewa fedha zao ambazo zilidhulumiwa na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kutokomeza vitendo vya rushwa Wilayani humo.