Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI ikiongozwa na makamu Mwenyekiti, Justine Nyamoga imeuelekeza Uongozi wa Mkoa wa Tabora kuzigatia ushauri wa kitaalamu wa kihandisi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu.

Nyamoga ameyasema hayo katika majumuisho baada ya ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya Elimu kupitia program ya BOOST na SEQUIP iliyotekelezwa katika Mkoa wa Tabora.

Ziara hiyo ya siku mbili katika mkoa huo imefanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Halmasauri ya Wilaya ya Urambo na Halmashauri ya Wilaya ya Uyui.

Amesema, “maelekezo ya Kamati ni kwamba ujenzi wowote wa miradi uzingatie ushauri wa kitaalamu wa wahandisi ambao unajali muda, ni bora usubiri ujenge jengo bora kuliko kujenga jengo lenye uhafifu kwa mamilioni ya fedha,” alisema Nyamoga.

Aidha, Nyamoga amezitaka Halmashauri kuzingatia maelekezo na utaratibu wa matumizi ya mapato ya ndani katika ukarabati na ukamilishaji wa miundombinu ya miradi ambayo Fedha zake zimetoka Serikali kuu.

Awali akisoma Taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya Elimu kupitia program ya BOOST na SEQUIP, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt. John Mboya amesema Mwaka 2021/22 – 2023/24 Mkoa wa Tabora ulipokea jumla ya shilingi 59,444,003,381.00 zikijumuisha shilingi 16,729,200,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Elimu kupitia program ya BOOST na shilingi 42,714,803,381.00 ikiwa ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu kupitia program ya SEQUIP.

Naye Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Rais ya TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI imepokea maelekezo yote yalioyotolewa na Kamati na itasimamia utekelezaji wake.

Wawili mbaroni kwa kusambaza taarifa za uongo
Tunadi sera siyo chuki, uvunjifu wa amani - Dkt. Mwinyi