Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), imetekeleza agizo la Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew, la kuwaunganishia wananchi huduma ya Majisafi wa eneo la Stone Town Buswelu lililopo Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza.
Mhandisi Kundo, alitoa agizo hilo Julai 26,2024 kwa MWAUWASA ambapo aliipa Mamlaka hiyo siku 14 ihakikishe wananchi wa eneo hilo wameunganishwa na huduma ya maji.
Agosti 10, 2024, Mhandisi Kundo alitembele eneo hilo na kushuhudia nyumba kadhaa zikiwa tayari zimeunganishiwa huduma ya maji na huku zoezi la kuwaunganishia wananchi likiendelea kutekelezwa na mafundi wa MWAUWASA.
Aidha, amesema kuwa mwelekeo wa Wizara ya Maji chini ya Waziri wa Maji Jumaa Aweso ni kuhakikisha kila Mwananchi anafikiwa na huduma ya Majisafi na Salama kama ilivyo adhma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
“Naendelea kumshukuru na kumpongeza Mhe. Waziri wa maji, Jumaa Aweso kwa kutoa miongozo thabiti ya kuhakikisha Watanzania wanapata Majisafi na Salama, na haya yote yanatokana na kwamba kazi kubwa ya kumtua mama ndoo kichwani iliyoasisiwa na Mhe. Rais imekabidhiwa kwake, hivyo sisi wasaidizi wake kazi yetu ni kuhakikisha tunamsaidia Mhe. Waziri kutimiza majukumu aliyokabidhiwa na Mhe. Rais,” amesema.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kundo ameipongeza MWAUWASA kwa kutekeleza agizo hilo kwa wakati na kuwaeleza wananchi kuwa licha ya kuunganishiwa huduma hiyo, MWAUWASA itaendelea kutoa huduma kwa kutekeleza migao wakati miundombinu ya uzalishaji na usambazaji maji ikiendelea kuimarishwa.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula amepongeza kazi inayofanyika na kuiomba Serikali kupitia Wizara ya Maji kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati, ili kuimarisha zaidi huduma ya maji kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza.
Nao baadhi ya wakazi wa eneo hilo wakizungumza kwa nyakati tofauti wamepongeza kazi iliyofanyika na kutoa hamasa kwa wananchi wengine kuendelea kuunga mkono jitihada hizo za Serikali kwa kutunza miundombinu ya maji na kulipa bili za maji kwa wakati.