Warrior Queens yapongezwa ushiriki Klabu Bingwa Afrika

Watekelezaji wa program ya Michezo kwa Maendeleo Zanzibar (S4D) wamewatakia
heri timu ya Warrior Queens ya Saateni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika kwa upande wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), yanayotarajiwa kufanyika nchini Ethiopia kuanzia Agosti 17-31, 2024.

Warrior Queens qmbayo itaiwakilisha Zanzibar katika mashindano hayo, inatarajiwa
kuondoka nchini kuelekea Ethiopia Agosti 15, 2024 huku ikiaminiwa kuwa itaiwakilisha Zanzibar kwa fahari kubwa na kurudi nyumbani wakiwa washindi.

Pamoja na kuwapongeza, wadau waliofanikisha timu hiyo kukamilisha mahitaji yao ya
safari, TAMWA ZNZ imewasisitiza wadau wote kuendeleza usawa wa kijinsia kwa kuzisaidia timu za wanawake na kukuza vipaji vyao ili kujenga jamii inayothamini na kuinua michango ya wanawake.

Taarifa imeeleza kuwa bado ipo haja kwa wadau wote wa michezo, ikiwemo serikali, taasisi binafsi na wadau wengine kuongeza nguvu katika kuzisaidia timu za wanawake ili kuwawezesha wachezaji wetu wa kike kushiriki na kushinda mashindano mbalimbali, ndani na nje ya nchi.

Kufuzu kwa klabu ya Warriors Queens kwenye mashindano hayo, kunatokana na klabu hiyo kuchukua ubingwa wa ligi kuu soka Zanzibar upande wa wanawake msimu wa 2023/2024 ambapo jumla ya timu 10 za wanawake zilishiriki.

Program ya S4D inatekelezwa kwa mashirikiano na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake
Zanzibar (ZAFELA), Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD), kwa mashirikiano makubwa
na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Ujerumani – (GIZ) – chini ya Wizara ya
Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ).

Zanzibar: Gharama za uendeshaji miradi kupatiwa unafuu
Azam FC washitukia mbinu za Yanga