Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba na Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Christine Mwakatobe wamekutana hivi karibuni jijini Arusha kujadili hatua za maandalizi ya Kongamano la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki, litakalofanyika kwenye Ukumbi huo wa kimataifa, Septemba 9 – 12, 2024.

Viongozi hao walifurahia hatua za maandalizi zilizofikiwa na pande zote mbili, katika kuhakikisha kuwa kongamano hilo litakalofunguliwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuhudhuriwa na washiriki wa nchi zaidi ya nane linafanikiwa kwa hadhi ya kimataifa.

“Maandalizi yanaenda vizuri, kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Arusha tunahakikisha tukio hili linakuwa la kipekee na lenye hadhi ya kimataifa, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameliheshimisha zaidi kwa kukubali kulifungua na kuzindua Mfumo wa NeST,” amesema Mkurugenzi Mkuu, Simba.

“Wadau wa ununuzi wa umma na sisi tuna jambo letu. Tunahitaji Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla itambue Tanzania kuna tukio kubwa linalowahusu wadau wa ununuzi wa umma na washiriki wote wafurahie mazingira, mijadala na mambo mengine mazuri ya Tanzania,” Bw. Simba ameongeza.

Naye Mkurugenzi Mtendajiw a AICC, Mwakatobe alisema kuwa uongozi wa taasisi hiyo unahakikisha mazingira ya ukumbi na huduma nyingine ziko katika hali nzuri wakati wote, kwani lengo ni kuileta dunia Tanzania.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wengine wa taasisi hizo ambao kwa Pamoja walieleza kuridhika na maandalizi, wakiwataka washiriki kujisajili kupitia tsms.ppra.go.tz kwani nafasi ni chache na adhimu.

Kaulimbi ya Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki ni “Digitalization for Sustainable Public Procurement” (Matumizi ya Dijitali kwa Ununuzi wa Umma Endelevu).

Wakili Chikulupi: Nchi zetu zitafanya Biashara bila vikwazo
Tanzania, China kuimarisha biashara ya Mifugo, Uvuvi