Chama cha wafanyakazi wa serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimeipongeza Serikali kwa kupokea na kutekeleza mapendekezo mbalimbali waliyoyapeleka.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa TALGWU, Rashid Mtima wakati wa mkutano wake na Wanahabar jijini Dar es Salaam ambaye amesema wameridhishwa na utendaji kazi wa serikali ya awamu ya sita katika kutatua kero mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili kwa muda mrefu ikiwemo suala la wanachama wake kulipwa mishahara yao kupitia mapato ya ndani.
Rashid Mtima amesema Wanachama wa TALGWU wapatao 645 kutoka halmashauri mbalimbali nchini walikuwa wanalipwa mishahara kupitia mapato ya ndani ya halmashauri. Wao kama chama walianza majadiliano mbalimbali na serikali kuzungumzia changamoto, kero na kadhia kubwa wanazopitia wanachama wake.
Hivyo, waliiomba serikali kuwalipa mishahara wanachama hao kupitia mfuko mkuu wa Serikali (HAZINA), ili kuwaondolea changamoto kubwa zilizokuwa zinawakabili.
Mtima amesema changamoto hizo ni pamojq na Wanachama wake kutolipwa mishahara yao kwa wakati, kukosa huduma za matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutokana na makato kutowasilishwa kwa wakati.
Nyingine ni kutokukopesheka katika baadhi ya taasisi za kifedha, kupata usumbufu mkubwa kipindi wanapo staafu kutokana na makato ya michango yao kutokuwasilishwa kwa wakati katika Mfuko wa hifadhi ya jamii.
Aidha, TALGWU imeishukuru serikali kwa kuridhia na kuanza utekelezaji wa maombi hayo, kuanzia Julai 2024 jumla ya wanachama 465 Kati ya 645 walianza kulipwa kupitia Mfuko mkuu wa Serikali (HAZINA) . Mpaka sasa chama hicho kimebakiza wanachama 180 pekee ambao bado wanaendelea kulipwa na halmashauri za majiji na manispaa.
Hata hivyo, imeiomba Serikali iwasimamie Wakurugenzi wa Halmashauri za majiji ya Mbeya , Mwanza, Ilala na Dodoma pamoja na Manispaa za Kinondoni, Temeke, Geita na Morogoro kulipa mishahara kwa wakati kama ambavyo inafanya HAZINA, ili wanachama wake 180 waweze kuondokana na changamoto hizo na hii itawasaidia kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa tofauti na sasa wanapowekwa katika matabaka.