Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko leo Agosti 15, 2024 ameshiriki kikao cha 19 cha pamoja cha Mawaziri wa Nishati ambao ni Wanachama wa Umoja wa soko la pamoja la kuuziana umeme na kuimarisha mifumo ya Gridi ya EAPP (Eastern Africa Power Pool) unaofanyika nchini Uganda.
Mkutano huo, unajadili masuala mbalimbali ikiwemo kupitisha mabadiliko ya mikataba ya uongozi wa EAPP, kuridhia kanuni za uanzishwaji wa kitengo kinachojitegemea cha kusimamia soko la biashara ya umeme kwa nchi wanachama (Marketing and Trading unit) na kuridhia kanuni na taratibu za uendeshaji wa vikao vya Baraza la Mawaziri, Makatibu wakuu, na kamati ya uongozi.
Umehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Dennis Londo, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, Mkurugenzi wa Shirika la Umeme (TANESCO) Mha. Gissima Nyamo-Hanga, Naibu Mkurugenzi Mipango, utafiti na uwekezaji, CPA. Renatha Ndege, Viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na taasisi zake.