Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesema maboresho ya Kanuni na Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii – CSR, za Mwaka 2023 yamelenga kuhakikisha kunakuwa na ushirikishwaji wa pamoja kati ya jamii na Kampuni za Madini katika utekelezaji wa miradi ya jamii.
Dkt. Kiruswa ameyasema hayo wakati akifungua Kikao cha maboresho ya Kanuni hizo jijini Dodoma kilichowashirikisha Wadau, Wataalam kutoka Halmshauri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri Taasisi za Umma, Vyama vya Wachimbaji na Asasi za kiraia.
Amesema, tangu mwaka 2017, baada ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kufanyiwa marekebisho na kuongezwa kifungu cha 105 kinachohusu wajibu wa Kampuni kwa jamii, Sekta ya Madini imeona mafanikio makubwa na kwamba licha ya mafanikio hayo, utekelezaji wa Kanuni za CSR umekuwa na changamoto kadhaa ambazo zinahitaji kushughulikiwa kupitia maboresho.
“Ndugu Washiriki, changamoto hizo ni pamoja na Mipango ya miradi ya CSR kutoandaliwa kwa wakati na ile miradi iliyoandaliwa kutotekelezwa kwa wakati; Kukosekana kwa miongozo ya utekelezaji wa mipango ya CSR ambayo kwa mujibu wa Sheria inapaswa kuandaliwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kuwashirikisha Wamiliki wa Leseni za Madini,” alisema Dkt. Kiruswa.
Aidha, metaja changamoto zingine kuwa ni kupishana kwa mitazamo kati ya Halmashauri na Wamiliki wa Leseni za Madini kuhusiana na aina ya miradi na namna ya kuitekeleza pamoja na uelewa mdogo wa masuala za CSR kwa jamii pamoja na migogoro baina ya Wamiliki wa Leseni za Madini na Mamlaka za Serikali za Mitaa hali inayopelekea baadhi ya miradi ya kijamii kutokukidhi mahitaji na matarajio ya jamii zinazozunguka migodi.