Johansen Buberwa – Kagera.
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera imefanikiwa kuvuka lengo la makusanyo ya mapato ya ndani ambapo zaidi ya shilingi bilioni 8.6 sawa na asilimia 125 ya lengo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Justus Magongo amesema hayo kwenye kikao cha baraza la Madiwani cha kujadili taarifa ya robo ya nne ya mwaka wa fedha ambacho kimefanyika Agosti 16,2024 katika ukumbi wa Halmashauri.
Magongo amesema kuwa awali walikuwa wamelenga kukusanya shilingi bilioni 6.5 hivyo kutokana na ushirikiano wa Madiwani na watumishi wa Wilaya hiyo wameweza kuvuka lengo na fedha hizo ambazo zinaendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga amelitaka baraza la madiwani kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuendelea kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Katika hatua nyingine Dkt. Nyamahanga amewataka Madiwani kuendelea kusimamia swala la lishe mashuleni ili kuondoa hali ya udumavu kwa watoto ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya lishe kwa wazazi na walezi wao.
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, wakuu wa taasisi, Kamati ya usalama ya wilaya na viongozi wa dini.