Mratibu wa mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP), Richard Makota amewataka washiriki kuyaishi kwa vitendo Mafunzo waliyopatiwa kwa muda wa siku tatu kuhusu Mpango wa utekelezaji wa Shule salama ili dhamira ya Serikali ya kuwepo Usalama mashuleni kutimia kwani lengo la Serikali imeanzisha Mpango wa Shule Salama katika shule za sekondari nchini ni kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na kuongeza ulinzi na usalama wa watoto.
Ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo maalum ya siku tatu ya Mpango wa Shule Salama, yaliyowakutanisha washiriki kutoka mikoa ya mtwara, Lindi, Tabora, Pwani na Dar es salaam yakijielekeza katika kuwajengea washiriki uwezo na mbinu zitakazo leta mabadiliko ili kuhakikisha shule za sekondari zinakuwa salama.
Mafunzo haya yamehusisha wenyeviti wa bodi za shule za sekondari, maafisa kutoka ngazi za mikoa, maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata, pamoja na waratibu wa Mpango wa Shule Salama.
Naye mratibu wa Mpango wa Shule Salama kupitia Mradi wa SEQUIP kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Hilda Mgomapayo akizungumza na washiriki wa mafunzo ya utekelezaji wa Mpango wa Shule Salama wakati wa kuahirisha mafunzo hayo amesisistiza kuwa wenyeviti wa bodi na washiriki wengine ni viungo muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanalindwa ndio maana Serikali kupitia Mpango wa Shule salama wameona umuhimu wa kuendesha mafunzo hayo.
Aidha, ameweka mkazo katika suala la ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika upangaji,utekelezaji na tathimini ya Mpango wa Shule salama kwa vitendo.