Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amewataka wananchi wa Wilaya ya Bahi na Tanzania kwa ujumla kutambua umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji, ili huduma ya maji safi na salama iweze kuwa endelevu.
Dkt. Mpango ametoa wito huo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Bahi mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Mradi wa Maji Ibihwa akiwa ziarani mkoani Dodoma.
Amesema, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya pia wanatakiwa kuwaongoza Wananchi kupanda miti rafiki kwa vyanzo vya maji hususani wakati wa kipindi cha mvua.
Aidha, Dkt. Mpango ameitaka Tume ya Umwagiliaji kufanya kazi ya ziada kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo kutengeneza mabwawa ya kuvuna maji katika Mkoa huo kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji, mahitaji ya mifugo na binadamu.
Ameiagiza pia Wizara ya Maji kuhakikisha asilimia 14 za ujenzi wa mradi wa maji Ibihwa zilizobaki zinakamilishwa ifikapo mwisho wa mwezi Septemba 2024.