Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika – TLS, limeunda Kamati maalum ya kufuatilia sakata la Ngorongoro na kuwasiliana na Idara, Wizara na Vyombo vyote vinavyohusika na suala la eneo hilo ili kujua ukweli na kuhakikisha kunakuwepo na uzingatiaji sheria.
Rais wa Chama hicho, Wakili Boniface Mwabukusi amesema Kamati hiyo inayotarajia kumaliza kazi ndani ya kipindi cha siku 30, inajumuisha Wajumbe akiwemo Dkt. Rugemeleza Nshala, Tike Mwambipile, Bumi Mwaisake, Laetitia Petro Ntagazwa na Paul Kisabo.
Amesema, pia Kamati itafanya mashauriano na Taasisi mbalimbali pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo yenye migogoro, ili kujua uhalisia.
“Kamati pia itafanya mapitio ya Sera, Sheria na Mazoea na kuzichambua kuhusiana na umiliki wa ardhi kwa Wazawa pamoja na shughuli za uwekezaji na uhifadhi na kubaini uzingativu wa haki za msingi za Raia katika maeneo husika kwa kuzingatia Katiba, Sera na Sheria za Nchi,” alisema Wakili Mwabukusi.