Makamu wa Rais wa Nigeria, Kashim Shettima ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya Nigeria na Tanzania, akisisitiza umuhimu wa ujumuishaji wa kikanda na juhudi za pamoja ili kufanikisha ukuaji na umoja wa bara.
Maoni hayo yametolewa wakati wa mkutano na Rais wa zamani wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, katika Ikulu ya Rais, Abuja ambapo Makamu wa Rais Shettima alibainisha kwamba nchi zote mbili zina uhusiano wa muda mrefu, hasa kama nchi za mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukoloni.
Alisisitiza haja ya kujenga juu ya historia hii ya pamoja ili kukuza uhusiano imara wa kiuchumi na kijamii, hasa ndani ya mfumo wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
“Tanzania ni moja ya hadithi za mafanikio za Afrika,” alisema Shettima, akilipongeza Taifa hilo kwa uongozi wake. “Kuanzia Julius Nyerere hadi Samia Suluhu Hassan, Tanzania imebarikiwa na viongozi bora. Taifa hili ni mfano wa matumaini na utulivu katika Afrika Mashariki.”
Makamu wa Rais huyo wa Nigeria alionesha furaha kwa kugundulika kwa akiba kubwa ya gesi, akisema kuwa Tanzania iko kwenye njia ya maendeleo ya haraka, jambo ambalo linafungua fursa za ushirikiano wa kina kati ya mataifa haya mawili.
“Iwapo mataifa muhimu ya Afrika kama Nigeria na Tanzania yatapata mafanikio, bara zima litanufaika,” aliongeza.
Mhe. Shettima pia aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kuunga mkono biashara za Nigeria zinazofanya kazi ndani ya mipaka yake, akitaja mafanikio ya kampuni kama United Bank for Africa, Guarantee Trust Bank, na Dangote Group.
Alisisitiza uwezekano wa kuongezeka kwa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili, jambo ambalo litazidi kuimarisha uhusiano wao wa kiuchumi.
Akijibu, Rais wa zamani Kikwete alielezea utayari wa Tanzania kuimarisha uhusiano wake wa kibiashara na kidiplomasia na Nigeria, na kwamba anatambua umuhimu wa urafiki kati ya mataifa haya mawili na akasisitiza dhamira ya Tanzania ya kuzidisha uhusiano huo.