Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amezitaka Hospitali zote na vituo vya Afya nchini kuhudumia wagonjwa wa nje wanaofika kupata huduma kwa masaa yasiyozidi matatu.
Waziri Jenista amesema hayo wakati alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ili kuona hali ya utoaji wa huduma sambamba na kuongea na watumishi waliopo Hospitalini hapo.
Amezitaka Hospitali zote nchini na kuziagiza kuzingatia mzunguko wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa na kuhakikisha mzunguko huo unatumia masaa ya kitaalamu ambayo hayazidi masaa matatu kwa kila mgonjwa na kupunguza muda wa wagonjwa kukaa Hospitali kusubiri huduma.
Ameongeza kuwa muda huo ni kuanzia mgonjwa anapofika hospitalini kwa kuanza kujiandikisha, kumuona daktari, wakati anapatiwa matibabu na kupatiwa dawa kwamba mzunguko huo wa mgonjwa usizidi masaa matatu.
Ili kufanikisha hilo Waziri Mhagama amesisitiza uwepo wa matumizi ya TEHAMA pamoja mifumo kusomana ikiwa njia ndiyo njia pekee ya kuokoa muda na kutoa huduma bora kwa mgonjwa ikiwa ni sehemu ya kupunguza malalamiko ya mara kwa mara.