Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania – TMA, imeotoa angalizo juu ya uwepo wa mvua za kusuasua zitakazotawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko usioridhisha katika maeneo mengi.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2024 katika ukanda wa ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Octoba, 2024 na zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Desemba, 2024

Amesema licha ya maeneo mengi kutarajia kupata mvua za chini ya wastani pia kutakuwepo na matukio ya vipindi vifupi vya mvua na joto kali kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Dkt. Chang’a, amesema miongoni mwa athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na upungufu wa unyevunyevu kwenye udongo na ongezeko la wadudu na magonjwa katika mazao.

Dkt. Chang’a ametoa tahadhari kwa wakulima kutumia teknolojia ya kuhifadhi maji kwenye kilimo ili kukabiliana na hali hiyo.

Amesema kwa ukanda wa ziwa Victoria unaojumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza Shinyanga, Mara na Simiyu zinatarajia kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani zitakazoanza mwezi wa Septemba na kuisha Disemba

Kwa ukanda wa nyanda za Kaskazini Mashariki unaojumuisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara pia inatarajia kupata mvua za chini ya wastani hadi za wastani na zinatarajia kuanza wiki ya tatu ya Mwezi Oktoba na kuisha mwezi Disemba.

Kwa upande wa Ukanda wa Pwani Kaskazini unaojumuisha Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam Pwani na Visiwa vya Mafia na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba zitapata mvua zilizo chini ya wastani hadi wastani na mvua zinatarajia kuanza mwezi Oktoba hadi Disemba.

Sambamba na hayo ametoa wito kwa Jamii kuchukua tahadhari za utunzaji Maji hususani maeneo ya mgodini ambapo hutumia kiasi kikubwa Cha maji kwani uwepo wa mvua za wastani na chini ya wastani kutasababisha upungufu wa Maji. @tanzaniameteorological

Zuio la Mahakama Ngorongoro: Taratibu za uchaguzi kuendelea
Kambi ya masomo: Shule tano zakabidhiwa Chakula Msoga