Novemba 16, 2020 wakati wa kuapishwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Fedha wakati huo, Dkt. Philip Mpango (sasa Makamu wa Rais), Prof. Palamagamba Kabudi alitoa kanuni nane kuhusu cheo na mahusiano na bosi.
Kanuni hizi alisema zinafaa kuandikwa kwa wino wa dhahabu na kuwa dira ya viongozi, wanaowania uongozi na mahusiano yako na Kiongozi wako.
1. Usiwaruhusu watu wakuandae kwa cheo chochote na hasa kama hawana mamlaka ya uteuzi wala hawaamui kwa kura zao kwani utafadhaika na kuishi maisha ya shida.
2. Usijiandae kwa cheo chochote maana ukipata utakuwa na kiburi na fahari na ukikosa utamchukia yule aliyepewa wakati vyeo ni kudra ya Mungu.
3. Ukiwa msaidizi wa mtu usijione uko sawa au juu yake. Hii ni kwa sababu atakuwa anakupa mambo magumu na mazito uyatatue. Kama huna hekima na busara utaona kama mko sawa au uko juu yake.
4. Ukiwa msaidizi wa mtu jua kimo chako na ujue mipaka yako na hivyo muda wote heshimu mipaka yako.
5. Fanya kazi kwa bidii lakini mazuri yote ni ya bosi wako na mabaya yote yabebe wewe.
6. Kila mara tilia maanani kwamba kiongozi mkuu hazoeleki na ‘make sure’ humzoei.
7. Mshauri bosi wako kwa kiasi. Akiamua tofauti na ushauri wako msikilize na usinune. Badala yake tekeleza uamuzi kama vile hukuwahi kumshauri chochochote.
8. Ushauri wako ukitekelezwa na bosi wako usitoke ukaenda kutamba kwa mkeo au mumeo.
Kanuni hizo bila shaka ni muongozo wa ziada katika kuaishi maadili ambayo ni mafundisho yanayotolewa katika nafasi mbalimbali, hasa katika malezi, ili kuelekeza binadamu atende namna ambayo itamjenga yeye na jamii nzima.
Kimsingi maadili yanayohitajiwa na watu wote ni yaleyale, lakini mazingira yanaweza kudai yatekelezwe kwa namna tofauti, kwani tangu zamani Watu waliyaishi maadili kulingana na dini, utamaduni, falsafa n.k.
@grasonnyakarungu