Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema atasimamia shabaha ya kuwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) madhubuti na lenye Maafisa na Askari wenye weledi, ari na zana bora.

Dkt. Samia ameyasema hayo wakati akifunga Zoezi la Medani katika kuadhimisha Miaka 60 ya JWTZ katika eneo la Pongwe Msungura, lililoko Msata Agosti 23, 2024.

Aidha, amesisitiza kuwa Jeshi imara zaidi litatokana na dhamira ya kweli, moyo wa kujituma na uchumi imara zaidi na kuitaka JWTZ kuendelea kulinda misingi ya kuanzishwa kwa Jeshi hilo na kuendelea kudumisha nidhamu, utii, uaminifu na uhodari uliopo katika Jeshi hilo.

Rais Samia pia amesisitiza JWTZ kuendelea kuwa Jeshi la Wananchi la ukombozi la mfano kwa Afrika na Dunia kwa namna linavyoonesha uhodari, weledi na nidhamu ya kijeshi.

Ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kushirikiana na JWTZ katika Zoezi la Medani lililojumuisha mazoezi ya baharini na nchi kavu. Aidha, amepongeza ujio wa meli kubwa ya hospitali ya kijeshi iliyotoa huduma ya vipimo na matibabu kwa wananchi takribani 8,000.

Kupitia mazoezi hayo, JWTZ imebadilishana uzoefu kuhusu mbinu mbalimbali za kupambana na ugaidi, uvuvi haramu, uharamia, usafirishaji haramu wa watu na madawa ya kulevya.

Collina: Amka upigane bado una sekunde 20
Siri ya kubaki kuwa Viongozi bora wa wakati wote