Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amepokea gawio la Serikali la zaidi ya Shilingi Bilioni 4.35, kutoka Kampuni ya Bomba la Kusafirisha Mafuta la Tanzania – Zambia (TAZAMA).
Dkt. Biteko amepokea gawio leo Agosti 26, 2024 jijini Dar es Salaam huku akishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa nchi hizo mbili ambapo ni miaka mitano tangu kutolewa kwa gawio mwaka 2019.
Amesema mapokezi ya gawio hilo ni matokeo ya ziara ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan nchini Zambia ambapo alielekeza miradi isimamiwe vizuri ili ilete matunda na kubadili maisha ya watu wa nchi hizo mbili.
Aidha, ameitaka TAZAMA kuendelea kulisimamia vizuri Bomba hilo ili lizidi kuleta faida ambapo mikakati iliyopo sasa ni kuongeza ukubwa wa bomba la TAZAMA kutoka inchi nane hadi inchi 12.
Pia, amesema kuwa, Serikali za nchi hizo mbili ziko katika hatua za manunuzi kwa ajili ya kujenga bomba kubwa la mafuta lenye kipenyo cha inchi 24, suala litakalopunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa hiyo, ikiwa ni pamoja na kulinda miundombinu yake.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo ameeleza kuwa Kampuni hiyo iliyokuwa kwenye hati ya kufa imeonesha kufufuka na kutoa gawio kwa Serikali.
“Tumezoea Watu na Mashirika yakiomba pesa kwa Serikali, lakini leo ni kinyume na tunashuhudia Serikali ikipokea gawio, hilo ni jambo la kujivunia sana.” Amesema Prof. Mkumbo.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema kwa umri wa Kampuni ya TAZAMA yenye miaka 58 tangu kuanzishwa kwake imeonesha matumaini makubwa kwa kuanza upya kutoa gawio kwa Serikali na hii ni kutokana na utekelezaji wa 4R za Rais Samia Suluhu Hassan.