Klabu ya Azam FC itarejea dimbani siku ya jumatano kuvaana na JKT Tanzania. Huu utakuwa ni mchezo wa kwanza kwa klabu hiyo tangu kuanza msimu mpya wa ligi kuu ya NBC. Azam FC walishindwa kucheza michezo miwili ya awali kutokana na ratiba ya CAF iliyowakutanisha na APR ya Rwanda hatua za awali kufuzu hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika.
Azam waliondoshwa katika michuano hiyo kwa jumla ya mabao 2-1.Wakipata ushindi wa bao 1-0 mchezo wa kwanza uliopigwa dimba la Azam Complex jijini Dar es salaam na walipoteza mchezo wa pili kwa mabao 2-0 mchezo uliopigwa dimba la Amahoro Stadium jijini Kigali nchini Rwanda. Kikosi cha kocha Yusuph Dabo kitaanzia mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya NBC ugenini dhidi ya Maafande hao na kitakwenda mapumziko kupisha michezo ya timu ya taifa itakayopigwa kati ya tarehe 4 mpaka 10 Septemba.
Azam FC imetoa wachezaji watano kwenye kikosi cha timu ya Taifa Stars ambao ni Lusajo Mwaikenda ,Nathaniel Chilambo,Pascal Msindo ,Adolf Mtasingwa na Feisal salum. Wachezaji hao watajiunga na kambi ya Taifa Stars mara baada ya mchezo huo.
Hatma ya Makocha wa Azam baada ya kupoteza mchezo dhidi ya APR
Klabu ya Azam FC haijatoa taarifa zozote kuhusiana na makocha pamoja na benchi la ufundi mara baada ya klabu hiyo kuondoshwa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Afrika na APR .Mashabiki wengi walionekana kuchukizwa na namna timu hiyo ilivyocheza mchezo wake wa pili dhidi ya APR na wengi walimshutumu kocha Yusuph Dabo hatoshi kuendelea kuiongoza Azam FC. Kwa upande wa Uongozi wa Azam bado unaimani na kocha huyo kwa sababu kuu mbili ,Kwanza alifanikiwa kumaliza nafasi ya pili ligi kuu ya NBC na CRDB Cup kwa msimu wa 2023/24 na pili amekuwa akionyesha mwelekeo chanya kwenye kikosi hicho kwa namna alivyotengeneza timu ya Ushindani, kama atakuwa na mwendelezo mzuri wa michezo ya ligi basi atasalia klabuni hapo.