Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ameagiza kufuatiliwa, kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua kwa watendaji wote walioshiriki kukwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na ofisi yake na kusababisha ishindwe kukamilika kwa wakati mkoani Kigoma.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo katika mahojiano maalum na waandishi wa habari Mkoani humo, wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku tatu ya kutemebelea na kukagua mwenendo wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maenedeleo inayotekelezwa chini ya ofisi yake.
Amesema katika ziara yake amebaini uwepo wa dalili za ubadhirifu na uzembe wa baadhi ya watumishi hali inayosababisha kuzorota kwa ujenzi wa baadhi ya miradi, hatua iliyomlazimu kuagiza timu ya ukaguzi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI kurejea maeneo yote aliyopita na kufanya ukaguzi wa fedha iliyotumika na thamani ya miradi iliyojengwa.
Akitolea mfano wa miradi yenye dalili za ubadhilifu, Waziri Mchengerwa ameitaja shule maalum ya Sayansi ya Wasichana Mkoani Kigoma inayojengwa wilayani Uvinza kama kiashiria tosha cha baadhi ya watendaji kushiriki kukwamisha jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kumuwezesha mtoto wa kike asome katika mazingira rafiki ili kutimiza ndoto zake.
“Shule hii ni moja kati ya shule 26 zinazojengwa kwenye kila mkoa wa Tanzania bara, kila shule ikigharimu zaidi ya shilingi bilioni nne nukta moja(4.1 😎, maalum kwa ajili ya kutoa fursa kwa Watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi na shule zote zilitakiwa kuwa zimekamilika kabla ya mwezi Julai 2024, lakini kwenu hapa Kigoma ndiyo kwanza mnajikongoja, kwenye hili lazima tufanye uchunguzi,” alisema Mchengerwa.
Aidha, liongeza kuwa, “Endapo itabainika kuna watu walihusika na ubadhirifu katika ujenzi wa mradi huu wa shule maalum ya wasichana Kigoma, wawe wamestaafu au wamehamishwa katika vituo vyao vya kazi lazima wakamatwe na wapelekwe mahakamani kujibu tuhuma hizi, ikiwa ni pamoja na kushindwa kuwajibika hadi kupelekea miradi kutokukamilika kwa wakati, hili litatumika kama onyo kwa sote tunaopata dhamana kuthamini pesa hizi ambazo ni kodi za watanzania.”
Katika ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi Mkoani Kigoma, Waziri Mchengerwa ametembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kigoma mjini, Kigoma vijijini, Kasulu mjini, na maeneo ya Kagerankanda Kasulu vijijini, pamoja na maeneo mbalimbali ya wilaya ya Uvinza.

Maisha: Kukosa hela ni tabia mojawapo ya Mwanaume
Busega: Serikali yaiongezea bajeti TARURA